Obama:Majeshi huenda yakatumwa Libya

Katibu mkuu wa NATO Anders Fogh Rasmussen Haki miliki ya picha Reuters (audio)
Image caption Wakuu wa NATO wanajadiliana kuhusu hatua za kuchukuliwa Libya

Serikali ya marekani imesema, ikishirikiana na majeshi ya NATO, inazingatia uwezekano wa kutumia nguvu za kijeshi kukabiliana na mzozo unaoendelea nchini Libya.

Rais Barack Obama ameongeza kuwa utawala wake utasimama imara na raia wa Libya ambao wanadai haki zao za kidemokrasia katika kipindi hiki.

Wakati huo huo, Mataifa ya kiarabu katika eneo la Ghuba yamelaani mashambulizi yanayoendelea dhidi ya raia wasio na hatia nchini humo. Viongozi hao wamelitaka baraza la usalama la umoja wa mataifa kupiga marufuku ndege za kijeshi kupaa katika anga ya Libya.

Uingereza imethibitisha kuwa inafanya kazi na washirika wake katika baraza la usalama la umoja wa mataifa kuhusu azimio la kupiga marufuku ndege kupaa katika anga ya Libya lakini Urusi imekariri msimamo wake wa kupinga makabiliano ya kijeshi.

Nchini Libya kwenyewe, vikosi vinavyoipinga serikali katika mji wa Ras Lanuf vimetimuliwa na wanajeshi walio watiifu kwa kanali Gaddafi.

Mashambulio ya angani yamelenga mji huo ambao ulitumiwa na wapiganaji wa upinzani kujikusanya katika harakati zao za kuelekea magharibi hadi mji mkuu, Tripoli. Watu wasiopungua ishirini wameripotiwa kuuwawa.

Televisheni inayomilikiwa na serikali, imeonyesha picha za wanajeshi wanaomuunga mkono Gaddafi wakiwa kwenye eneo inalosema ni mji uliokombolewa wa Bin Jawad, na ule wa Ras Lanuf.