Kesi ya ufisadi ya Bw Muluzi yaanza

Rais Bingu wa Mutharika
Image caption Rais Bingu wa Mutharika

Kesi ya aliyekuwa Rais wa Malawi Bakili Muluzi imeanza akituhumiwa kwa mashtaka ya ufisadi.

Mahakama Kuu ilikataa ombi lililotolewa Jumatatu kuzuia kesi hiyo kwa misingi ya hali ya afya ya Bw Muluzi.

Aliyekuwa Rais huyo ametuhumiwa kwa matumizi mabaya ya takriban dola za kimarekani milioni 11 zilizotoka kwa wafadhili wa kimataifa.

Amekana mashtaka hayo- na mara zote amekuwa akisema hayo yote yametokea kutokana na kutofahamiana na Bingu wa Mutharika ambaye alikuja kuwa Rais mwaka 2004 baada ya yeye kumaliza muda wake.

Bw Muluzi alikamatwa mwaka 2005 kwa madai ya kuhusika na ufisadi, lakini hivi karibuni kesi hiyo imekuwa ikicheleweshwa kutokana na afya yake.

Mwandishi wa BBC Raphael Tenthani aliyopo Blantyre alisema tangu ajiuzulu mwaka 2004, Bw Muluzi amefanyiwa upasuaji wa mgongo mara kwa mara.

Rais Mutahrika alikwaruzana na Bw Muluzi baada ya kuingia madarakani, na kumshutumu mwenziwe ambaye aliwahi kumwuunga mkono kwa kuharibu mpango wake wa kupambana na ufisadi.