Arsenal yaaga michuano Ubingwa wa Ulaya

Arsenal wakicheza 10 walishindwa kuparamia kizingiti cha Barcelona baada ya kwa mara nyingine kutolewa katika patashika za kuwania Ubingwa wa Ulaya, walipolazwa 3-1 kwenye mpambano ulioegemea upande mmoja katika uwanja wa Camp Nou usiku wa Jumanne.

Haki miliki ya picha 1
Image caption Robin van Persie akioneshwa kadi nyekundu

Kosa alilofanya nahodha wa Arsenal Cesc Fabregas, lilimzawadia Lionel Messi bao la kwanza alipoubetua mpira na kumpita mlinda mlango Manuel Almunia.

Arsenal walisawazisha kwa Barcelona kujifunga wenyewe baada ya Sergio Busquets kuutumbukiza mpira wavuni akijaribu kuokoa mpira wa kona, na muda mfupi baadae Arsenal walipata pigo baada ya Robin van Persie kutolewa nje kwa kadi nyekundu, kadi iliyoonekana na utata, baada ya Van Parsie kuupiga mpira wakati filimbi ya kuotea ilishapulizwa. Kabla ya hapo alikuwa ameoneshwa kadi ya njano.

Barcelona hawakusita kutumia nafasi hiyo ya Arsenal kucheza pungufu na gonga za hapa na pale zilimaliziwa na Xavi aliyefunga bao la pili, kabla ya Laurent Koscielny kumchezea rafu Pedro na Messi akatumbukiza bao la tatu wavuni kwa mkwaju wa penalti.

Heko kwa upande wa Arsenal zimuendee mlinda mlango wao Almunia aliyejitahidi kupunguza idadi ya mabao kwa kazi nzuri ya kupangua michomo ya karibu, hasa mkwaju wa Ibrahim Afellay na Messi, wakati Alves alikosa bao la wazi alipopiga mpira nje akiwa yeye na lango tu.

Mshambuliaji wa Arsenal aliyengia kipindi cha pili Nicklas Bendtner angeweza kuwaadhibu vinara hao wa La Liga baada ya kupokea pande zuri akiwa ndani ya sanduku la lango la Barca, lakini alianguka akijiandaa kufyatua kombora. Bao hilo lingetosha kuipeleka Arsenal hatua ya robo fainali.

Msimu uliopita Arsenal pia walitolewa na Barcelona katika mashindano kama haya, baada ya Messi kufunga mabao 4 peke yake na Arsenal walipata moja, na Barcelona walishinda kwa jumla ya mabao 6-3, baada ya mchezo wa awali timu hizo kutoka sare ya 2-2 katika uwanja wa Emirates.