Kesi ya Taylor ni 'ukoloni mamboleo'

Image caption Bw Charles Taylor

Wakili wa aliyekuwa Rais wa Liberia Charles Taylor alisema upande wa mashtaka umegeuza kesi yake ya uhalifu wa kivita katika " mfumo wa ukoloni mamboleo wa karne ya 21."

Courtenay Griffiths aliyasema hayo katika hitimisho ya utetezi wake kwenye mahakama maalum ya umoja wa mataifa ya Sierra Leone huko the Hague.

Bw Taylor ni aliyekuwa kiongozi wa kwanza barani Afrika kukabiliwa na kesi kama hii ya kimataifa.

Amekana kuhusishwa na mashtaka 11, ikiwemo mauaji, ubakaji, na kutumia watoto kuwa maaskari wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe Sierra Leone.

Anatuhumiwa kwa kuwapa silaha na kuwaongoza waasi wa Revolutionary United Front (RUF) wakati wa harakati za ugaidi kwa kipindi cha miaka 10 uliofanywa kwa kiwango kikubwa dhidi ya raia.

RUF ilivuma kwa sifa zake mbaya za kukata viungo vya mwili vya raia, na kutumia ubakaji na mauaji kutishia watu.

'Kwanini siyo Gaddafi?'

Katika hitimisho la upande wa utetezi, Bw Griffiths aliwaambia majaji kuwa wote watendewe haki sawa.

Aliuliza kwanini kiongozi wa Libya Kanali Muammar Gaddafi hayumo kwenye mahakama hiyo.

Alisema ni kwasababu serikali ya Uingereza iliyoongozwa na aliyekuwa waziri mkuu Tony Blair alitaka kufanikisha azma zake za kiuchumi na Libya.

Image caption Naomi Campbell

Wakili huyo wa utetezi pia alisema kwamba hakuna aliyeshughulikia kesi hiyo mpaka mwanamitindo maarufu Naomi Campbell na muigizaji wa Hollywood walipojitokeza, na tangu wakati huo ikabadilika kuwa kama haipo tena.

Bi Campbell na muigizaji Mia Farrow waliitwa kutoa ushahidi katika kesi hiyo mwezi Agosti.

Upande wa mashtaka ulikuwa ukijaribu kuweka uhusiano baina ya Bw Taylor na almasi ambazo hazikukatwa ambapo Bi Campbell alisema aligaiwa alipokuwa Afrika Kusini mwaka 1997.

Bw Taylor anatuhumiwa kuuza "almasi haramu zinazotumika kugharamia vita " kwa ajili ya waasi, ili na wao wapate silaha.

Upande wa utetezi ulisema Bw Taylor alijaribu kuleta amani Sierra Leone baada ya kuombwa na nchi jirani.

Kesi hiyo, inayofikia hatua za mwisho, ilicheleweshwa kwa wiki kadhaa kutokana na tofauti za kisheria, lakini wiki iliyopita upande wa utetezi ulishinda rufaa yake ili kutoa hitimisho.

Mwisho ilikuwa iwe Januari kwasababu ulisema ushahidi mpya uliibuka.

Mahakama maalum ya umoja wa mataifa ya Sierra Leone the Hague imesikiliza maelezo kutoka kwa zaidi ya mashahidi 100.

Kesi hiyo tayari imedumu kwa zaidi ya miaka mitatu na majaji wanatarajiwa kutoa uamuzi baadae mwaka huu.

Kama atakutwa na hatia, Bw Taylor atatumikia kifungo chake gerezani nchini Uingereza.