Usalama I Coast wazidi kuwa na utata

Haki miliki ya picha AP
Image caption Vijana wanaomwuunga mkono Ouattara

Raia wa Ivory Coast wanashuhudia ongezeko la silaha na mapanga kwenye mitaa ya mji wao mkuu, jambo ambalo limewatia wasiwasi wa nchi yao kuweza kurejea katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Kwa zaidi ya miaka minane nchi hiyo imegawika baina ya kaskazini, eneo linalotawaliwa na waasi na kusini ambako serikali inatawala.

Inaaminika kuwa jeshi lenyewe limegawanyika na habari za kuaminika zinasema kuwa wengi wa wanajeshi hao walimpigia kura Bw Ouattara.

Magharibi ya mbali ya nchi, vikosi vinavyomuunga mkono Bw Ouattara kutoka kaskazini mwa nchi vimeteka miji mitatu iliyo kwenye mpaka wa Liberia katika hatua inayoaminika kuwa ya kuzuia maharamia wasiingie nchini humo.

Lakini mbali na kutishia maeneo mbalimbali waasi wamesita kufanya shambulio kubwa la kuelekea kusini wakidai kuwa wanaheshimu mikataba ya amani - ambayo inaweza kubadili hali ya mazungumzo ya amani yanayoendelea na Umoja wa Afrika.

Labda wasiwasi mkubwa kwa Laurent Gbagbo ni ghasia zilizojitokeza mjini Abidjan, ambako sehemu kubwa ya wilaya ya Agogo imekuwa hatari hata kwa vikosi vya usalama.

Kambi ya Ouattara bado ina matumaini ya msaada wa kijeshi kutoka nje ya nchi labda kwa njia ya vikosi vya kimkoa kutoka shirikisho la ECOWAS.

Umoja wa Mataifa una takriban askari 10,000 wa kulinda amani ambao hadi sasa wameshindwa kuzuia machafuko.