Washukiwa wa Kenya kujibu mashtaka Hague

Moreno Ocampo Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Rais Kibaki anataka kesi dhidi ya washukiwa ihairishwe

Majaji wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC, huko the Hague Uholanzi wameamua kuwa wakenya sita wanaoshukiwa kupanga ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 wanahatia.

Washukiwa hao akiwemo naibu Waziri mkuu ambaye pia ni Waziri wa fedha Uhuru Kenyatta, mkuu wa utumishi wa umma Francis Muthaura na aliyekuwa Waziri wa Elimu ya juu, William Ruto wanatakiwa kufika mahakamani Aprili tarehe 7.

Wengine wanaokabiliwa na mashataka hayo ya mauaji, ubakaji na kuwalazimisha watu wahame makaazi yao ni aliyekuwa Waziri wa ustawi wa viwanda na mwenyekiti wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Henry Kosgey, aliyekuwa kamishna wa polisi Mohammed Hussein Ali na mtangazaji Joshua arap Sang.

Majaji Ekaterina Trendafilova na Cuno Tarfusser walikiri kuwa ushaidi uliowasilishwa mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo, Luis Moreno Ocampo umedhibitisha kuwa viongozi hao walihusika katika kupanga ghasia hizo. Hata hivyo jaji Hans-Peter Kaul hajakubaliana na wenzake.

Yamkini watu 1,500 waliuawa na maelfu wengine kutoroka makaazi yao hasaa katika mkoa wa bonde la ufa wakati wa ghasia hizo.

Bw Ocampo amewasilisha ushaidi kuhusu mauaji na uhalifu uliotokea katika maeneo ya Naivasha, Nakuru, Kisumu na Kibera.

Tangazo la mahakama hiyo, ni pigo kubwa kwa Rais Mwai Kibaki ambaye anataka kesi hizo ihairishwe.

Wiki iliopita alibuni jopo maalum la mawaziri likiongozwa na makamu wake, Kalonzo Musyoka, ambalo linajukumu la kushawishi baraza la uslama la umoja wa mataifa lishinikize mahakama ya ICC, ihairishe kesi hiyo dhidi ya washukiwa hao.