Ulaya yajadili upinzani wa Libya

Makundi ya kisiasa katika bunge la Ulaya yamekubaliana juu ya muundo wa azimio linaloutaka muungano wa Ulaya uanzishe mahusiano na baraza la mseto la Libya, ili kuhimiza hatua za kufikia utawala wa demokrasia nchini Libya.

Wabunge hao wanataka pendekezo hilo lijadiliwe kwenye mkutano wa kilele wa muungano huo mjini Brussels baadaye wiki hii.

Hatimaye kila nchi ina uhuru wa kujiamulia na viongozi watasita juu ya uamuzi wa kuunga mkono baraza la mseto nchini Libya wakati huu.

Hata hivyo uamuzi wa bunge hilo ni hatua muhimu kwa wajumbe wa baraza la mseto nchini Libya waliokwenda Strasboug kuomba msaada.

Katika mahojiano na BBC mmoja wa viongozi wa msafara wa baraza hilo Mahmoud Jibril amesema upinzani nchini Libya unahitaji msaada wa kila aina, kuanzia vifaa vya hospitali hadi vifaa vya kijeshi.