Uefa yawashitaki Wenger na Samir Nasri

Meneja wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger pamoja na mshambuliaji wa pembeni wa timu hiyo Samir Nasri, wameshtakiwa na Shirikisho la soka barani Ulaya- Uefa kutokana na matamshi yao makali dhidi ya mwamuzi baada ya kufungwa na Barcelona usiku wa Jumanne.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Arsene Wenger akibishana na mwamuzi Massimo Busacca

Msemaji wa Uefa amesema shauri hili linahusu mwenendo mbaya wa kocha na mchezaji.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Samir Nasri

Wanashtakiwa kwa kutumia "lugha mbaya" kwa mwamuzi Massimo Busacca baada ya mpambano wa usiku wa kuwania ubingwa wa Ulaya dhidi ya Barcelona.

Wenger alirushiana maneno makali na Massimo Busacca baada ya kichapo cha 3-1 na kutolewa kwenye mashindano ya Ligi ya Ubingwa wa Ulaya.

Wenger alikasirishwa na uamuzi wa kutolewa nje mshambuliaji wao Robin van Persie kwa kuoneshwa kadi ya manjano ya pili, wakati huo timu hizo mbili zilipokuwa nguvu sawa kwa kufungana 1-1 katika dakika ya 56.

Uefa imepitia ripoti ya mwamuzi Busacca kabla ya kuwashtaki Wenger na Nasri.