Congo ya ruhusu uchimbaji wa madini

Joseph Kabila Haki miliki ya picha AP
Image caption Waasi mashariki mwa nchi hiyo wanatumia faida ya madini kufadhili shughuli zao

Utawala wa Rais Joseph Kabila umeruhusu tena shughuli za kuchimba madini mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo baada ya kipindi cha miezi sita.

Rais Kabila aliweka marufuku hiyo ili kudhibiti biashara ya magendo ambayo imesababisha serikali kukosa kipato kutoka utajiri wake wa madini.

Uchimbaji na mauzo haramu ya madini hayo pia umekuwa ukichochea utovu wa usalama katika mikoa ya Kivu kaskazini na Kusini.

Waziri wa madini nchini humo, Martin Kabwelulu amesema kuwa harakati za kuwadhibiti waasi katika eneo hilo na mikakati ya serikali ya kuimarisha usimamizi wa shughuli za kuchimba madini ndio zimechangia marufuku hiyo kuondolewa.

Viongozi katika maeneo husika wameshirikishwa katika mikakati hiyo kuhakikisha kuwa utawala wa mikoa pia unafaidi kutoka kwa wawekezaji watakao sajiliwa kuchimba madini nchini humo.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inautajiri mkubwa wa madini yakiwemo, dhahabu, almasi na Kobalti yenye thamani kubwa kwenye soko la kimataifa.

Wiki iliopita Rais Kabila na mwenzake wa Kenya Mwai Kibaki walizindua tume ya pamoja itakayo endesha harakati za kudhibiti biashara ya magendo ya dhahabu.

Uchunguzi umeonyesha kuwa mtandao wa biashara hiyo ya magendo unaendesha shughuli zake nchini Kenya.