Hatma ya Ivory Coast itajulikana leo

wafuasi wa outarra Haki miliki ya picha Reuters
Image caption visa vya ghasia kati ya wafuasi wa viongozi hawa wawili vinaongezeka mjini Abidjan

Baraza la usalama la Umoja wa Afrika linakutana mjini Addis Ababa, Ethiopia kujadili hatua za kuchukuliwa baada ya juhudi za upatanishi nchini Ivory Coast kushindikana kwa mara nyingine.

Bw Alassane Outarra ambaye anatambulika kama mshindi wa uchaguzi uliofanyika Novemba mwaka jana, kwa mara ya kwanza amesafiri kutoka nchini humo kuhudhuria mkutano huo.

Lakini Rais Laurent Gbagbo ameususia na badala yake amemtuma kiongozi wa chama chake Bw Pascal Affi N'Guessan.

Baraza hilo litajadili ripoti ya jopo la viongozi watano walioteuliwa na Umoja huo kuongoza duru hii ya upatanishi kabla ya kutoa uamuzi wa hatua za kuchukuliwa kusuluhisha mzozo huo.

Jopo hilo linaongogzwa na Rais wa Mauritania Mohammed Ould Abdel Aziz. Wengine ni Jakaya Kikwete wa Tanzania, Jacob Zuma wa Afrika Kusini, Idriss Deby wa Chad na Blaise Compaore wa Burkina Faso.

Awali Umoja wa Afrika,ulitishia kutumia nguvu za kijeshi kumondoa Bw Gbagbo ambaye amekataa kuachia wadhifa wa urais.

Athari za vikwazo vya kiuchumi vilivyowekewa utawala wa Gbagbo zimeanza kusikika. Duru zinasema serikali sasa imeshindwa kulipa mishahara ya watumishi wa umma wakiwemo wanajeshi.