Wenger akana mashitaka

Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger amekana mashitaka yaliyotolewa dhidi yake na shirikisho la soka barani Ulaya Uefa, kufuatia matamshi aliyotoa kwa mwamuzi Massimo Busacca, katika michuano ya klabu bingwa Ulaya.

Image caption Arsene Wenger

Mshambuliaji wa Arsenal Robin Van Persie alipewa kadi nyekundu katika hali yenye utata, na baadaye Arsenal kupoteza 3-1 siku ya Jumanne, na hivyo kufanya matokeo baada ya mechi mbili kuwa 4-3 katika mchezo dhidi ya Barcelona.

Wenger alikasirishwa na kadi hiyo, na alishitakiwa kwa kutumia "lugha mbaya" dhidi ya mwamuzi kutoka Uswisi Busacca.

"Nakanusha vikali mashitaka yoyote. Hata sielewi yametoka wapi," amesema.

"Ingekuwa vizuri kwa Uefa kuonesha wamekosea, kuomba radhi kwakilichotokea, na sio kushitaki watu ambao hawajafanya makosa."

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Samir Nasri

Wenger na Samir Nasri walimkabili Busacca baada ya mchezo siku ya Jumanne. Nasri pia ameshitakiwa na Uefa.

Kikao cha nidhamu cha Uefa kitakaa tarehe 17 mwezi Machi.