Kanali Gaddafi azidi kuidhibiti Libya

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Libya

Majeshi yanayomtii kiongozi wa Libya Kanali Muammar Gaddafi yameripotiwa kufanikiwa kuwazidi nguvu waasi katika maeneo mawili muhimu.

Waandishi wa habari wa nchi za magharibi kwenye mji wa Zawiya, magharibi mwa Tripoli, walithibitisha madai ya utawala wa Gaddafi kuwa mji huo umedhibitiwa nao baada ya siku kadhaa za mashambulio.

Waasi wanasadikiwa kukimbia kutoka bandari ya Ras Lanuf kuelekea mashariki.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kujadili mgogoro huo, Uingereza na Ufaransa wakiongoza pendekezo la kuivamia nchi hiyo.

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron na Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy siku ya Alhamis walitoa wito wa kusimamishwa kwa ghasia dhidi ya raia haraka iwezekanavyo na Kanali Muammar Gaddafi na "magenge" yake kuondoka.

Lakini waliweka wazi kuwa hatua zozote zitakazochukuliwa na nchi za kigeni ikiwemo kupiga marufuku ndege kupita kwenye anga yao, itachukuliwa iwapo tu itaungwa mkono na jumuiya za kimataifa.

Mawaziri wa ulinzi wa jeshi la umoja wa nchi za kujihami za Ulaya Nato walijadili juu ya kuzuia ndege kupita siku ya Alhamis lakini wakaamua kunahitajika muda zaidi wa kujipanga.