Vinu vya nyuklia kuchunguzwa Ujerumani

Kiongozi wa Ujerumani, Angela Merkel, amesema usalama wa vinu vyote vya nyuklia nchini vitachunguzwa tena baada ya maafa yaliyotokea katika vinu vya Japan.

Image caption Bi Angela Merkel

Bi Merkel aliyasema hayo baada ya kufanywa maandamano makubwa kupinga matumizi ya nyuklia.

Hii ndio isahara ya mwanzo ya jinsi matukio ya Japan yanavyoweza kubadilisha majadiliano kuhusu matumizi ya nyuklia.

Matukio ya Japan yamebadilisha mawazo nchini Ujerumani.

Tayari kuna vuguvugu linalopinga kurefusha muda wa vinu vya nishati vya nuklia vilioko hivi sasa Ujerumani.

Maandamano yaliyofanywa jana yalihudhuriwa na maelfu ya watu.

Sasa kiongozi Angela Merkel amesema, "yaliyotokea Japan yataleta mabadiliko ulimwenguni, hasa kwa sababu Japan ni nchi iliyoendelea sana."

Aliongeza kusema kuwa, usalama wa vinu vya nishati vya nyuklia vya Ujerumani utachunguzwa tena ingawa alisema anaamini kuwa vinu vya Ujerumani ni salama.

Bila ya shaka, Ujerumani ni tofauti na Japan kwa sababu mitetemeko ni nadra.

Lakini hii ndiyo ishara ya mwanzo, kuonesha namna swala la nyuklia, litavyotazamwa katika nchi nyingi.