Ferguson awajibu Dalglish na Taylor

Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson amewajia juu Kenny Dalglish na Graham Taylor juu ya hulka yake dhidi ya waamuzi.

Image caption Ferguson na Dalglish

Ferguson anakabiliwa na mashtaka mbele ya Chama cha soka cha England-FA, baada ya kumshutumu mwamuzi Martin Atkinson baada ya Manchester United kufungwa mabao 2-1 na Chelsea.

Meneja wa Liverpool Dalglish na meneja wa zamani wa timu ya taifa ya England Taylor, walimtaka Ferguson aweke mawazo yake moyoni na si kusema ovyo.

Lakini Ferguson amesema "watu wana kumbukumbu fupi" na amesema yeye huamua kutosema lolote wakati mameneja hao wanapowashutumu waamuzi.

Baada ya kushuhudia Chelsea ikichukua pointi zote tatu katika uwanja wa Stamford Bridge mwanzoni mwa mwezi huu, Ferguson amesema mechi hiyo hiyo ilikuwa ikihitaji mwamuzi atakayechezesha kwa "haki" na alikuwa akitazamia "hali ingekuwa mbaya zaidi" mara tu baada ya kugundua mwamuzi atakuwa Atkinson.

Alipohojiwa baada ya mashtaka ya FA dhidi ya Ferguson ya utovu wa nidhamu kutokana na matamshi yake, Dalglish amesema yeye na wafanyakazi wengine wa klabu hiyo, wanaheshimu kampeni ya Kuheshimu ambayo inawataka mameneja kuwaunga mkono waamuzi.

Na Dalglish akaongeza: "Wakati mwengine unafikiri wale wanaopayuka zaidi ndio wananufaika na maamuzi na hiyo kwa kweli si haki."

Shutuma za Taylor dhidi ya Ferguson zilikuwa ni za moja kwa moja, akitumia gazeti la Daily Express akimuita "mnafiki" akadai wakati mwengine tabia yake si ya kutarajiwa na "mtu mwenye haiba kama yake".

Ferguson, hata hivyo amewashambulia wadau hao wawili wa soka ya England kutokana na shutuma dhidi yake.