Johan Djourou ahisi hajaumia sana bega

Mlinzi wa Arsenal Johan Djourou, anaamini hajaumia sana bega kama ilivyodhaniwa awali na ana matumaini ya kucheza tena mwezi huu.

Image caption Johan Djourou

Baada ya kuumia bega wakati wa mchezo wa robo fainali wa Kombe la FA, Arsenal walipofungwa na Manchester United siku ya Jumamosi, ilionekana hataweza kucheza tena hadi msimu huu utakapomalizika.

Lakini Djourou amekifahamisha Chama cha Soka cha Uswiss ana matumaini hatafanyiwa upasuaji na ataweza kucheza katika mechi ya kufuzu Kombe la Ulaya 2012 dhidi ya Bulgaria tarehe 26 mwezi huu wa Machi.

Mlinzi huyo mwenye umri wa miaka 24, majibu ya vipimo vya bega lake yatatolewa siku ya Jumanne.

Amepatiwa matibabu ya kutosha baada ya kuumia bega lake la mkono wa kuume, alipogongana na mwenzake Bacary Sagna wakati Arsenal ilipolazwa 2-0 katika uwanja wa Old Trafford.

Baada ya mechi hiyo, meneja wa Arsenal, Arsene Wenger alisema: "Kwa bahati mbaya tumempoteza Johan Djourou hadi msimu huu utakapomalizika - bega lake limechomoka - msimu kwake umekwisha."

Kutokana na hali hiyo, sasa Arsenal itawategemea Laurent Koscielny na Sebastian Squillaci kuwa nguzo pekee ya ulinzi wa kati, huku Thomas Vermaelen bado akisumbuliwa na matatizo ya kifundo cha mguu.

Djourou ana matumaini hajavunjika mfupa wowote katika kuumia kwake na iwapo kipimo kitaonesha hahitaji upasuaji, anaweza kuanza mazoezi mapema.