Tikiti za Olympik London zaanza kuuzwa

Tikiti kwa ajili ya michezo ya Olympiki ya London ya mwaka 2012 zimeanza kuuzwa, zikiwa zimesalia siku 500 kabla patashika hizo hazijaanza.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Eneo kulipozinduliwa mnara wa saa ya Olympiki

Kiasi cha tikiti milioni 6.6 zinapatikana kupitia mtandao wa London 2012 kwa kipindi cha wiki sita na waandaaji wamesema maombi yote yatashughulikiwa kwa njia sawa.

Bei za tikiti zinaanzia paundi 20 hadi 2,012 na michezo ambayo itakuwa na maombi mengi kushinda tikiti zilizopo, basi hizo zitauzwa kwa njia ya kura.

Siku ya Jumatatu, saa kubwa ya kuhesabu siku zilizosalia kabla michezo ya Olympiki haijaanza, ilizinduliwa katika eneo al wazi la Trafalgar Square mjini London.

Lord Coe, mwenyekiti wa London 2012, amesema: "Iwapo utaangalia namna tulivyoweka bei za tikiti pamoja, nadhani tumefanya hivyo kwa njia safi kabisa. Natumai bei zote hizo watu wanaweza kuzimudu.

"Ndio, michezo yenye kuvutia zaidi ndiyo itakuwa na gharama kubwa, lakini kuna kuna nafasi nyingi za kushuhudia mwanzo mzuri kwa tikiti za bei ya chini."

Lord Coe amesema ana matumaini makubwa tikiti zitanunuliwa na kumalizika.

Waandaaji wa mashindano hayo wamesema wanaimani wamefanya kila kitu wanachoweza kuepuka msongamano katika mtandao wakati watu watakapoingia kwa mara ya kwanza kununua tikiti.

Suala kubwa ni kuwekwa mchakato wa siku 42 za mauzo ya tikiti, ambazo zitakuwa na maana kila maombi yatakayopokelewa kuanzia sasa hadi tarehe 26 mwezi wa Aprili, yatashughulikiwa sawa.

Watu wanaweza kupeleka maombi kwa kutumia karatasi zitakazopatikana matawi ya Benki ya Lloyds TSB nchini England, Bank of Scotland ya Scotland ama maktaba zilizopo Ireland ya Kaskazini kati ya sasa na tarehe 15 mwezi wa Machi hadi tarehe 25 mwezi wa Aprili 2011.