Kasi ya Hernandez yamshangaza Ferguson

Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson amekiri kushangazwa na kasi ya ajabu inayozidi kukua ya Javier Hernandez, baada ya kuisaidia Manchester United kuiondoa Marseille katika mbio za kuwania Ubingwa wa Ulaya siku ya Jumanne.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Javier Hernandez

Mshambuliji huyo mwenye umri wa miaka 22, anayechezea pia timu ya taifa ya Mexico, alisajiliwa kutoka klabu ya Chivas de Guadalajara msimu uliopita, alipachika mabao yote mawili Manchester United walipoilaza Marseille 2-1 na kufuzu hatua ya robo fainali.

"Tumeshangaa," amesema Ferguson. "Tulipomnunua tulikuwa na wasiwasi itamchukua muda mrefu kuweza kuzoea.

"Ameweza kuzoea vizuri upande wa mikiki mikiki na anaweza kucheza muda wote wa dakika 90."

Hernandez aliipatia United bao la mapema la kuongoza katika dakika ya tano, katika mchezo huo wa marudiano wa timu 16, kwa mkwaju wa karibu ya lango baada ya kumalizia vyema pande kutoka kwa Wayne Rooney na katika dakika ya 75 akaunganisha tena pasi ya Ryan Giggs na kuandika bao la pili.

Marseille walijipanga upya kipindi cha pili na katika moja ya mashambulio yao makali, mlinzi wa United, Wes Brown akajishtukia anajifunga mwenyewe kutokana na kujichanganya na krosi ya Lucho Gonzalez, lakini Manchester United walihimili vishindi hivyo na kujihakikishia kucheza miongoni mwa timu nane zilizosalia.

Mabao hayo mawili ya Hernadez yamemuongezea hazina tangu ajiunge na timu hiyo kwa kufikisha mabao 16 katika mechi 33 alizocheza tangu alipotua Old Trafford.