Hatimaye ligi Misri kuanza Aprili 15

Ligi ya soka nchini Misri itaanza tena tarehe15 mwezi wa Aprili, baada ya kusimama kwa muda wa miezi mitatu kutokana na harakati za kimapinduzi zilizosababisha kuondoka madarakani aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Hosni Mubarak.

Image caption Mashabiki wa soka wa Misri

Chama cha soka cha Misri, kimesema ligi hiyo iliyoanza mwezi wa Agosti mwaka jana, sasa itamalizika tarehe 10 mwezi wa Julai.

Ligi ilisimamishwa mwishoni mwa mwezi wa Januari, kwa sababu ya maandano na ghasia mjini Cairo na miji mingine.

Taarifa hiyo imepokelewa kwa furaha na vilabu, ambavyo mapato yake yalikuwa yamekauka kwa kukosekana kwa ligi hiyo.

"Hili ni jambo tulilokuwa tukilisubiri kwa hamu kubwa vilabu vyote", mjumbe wa bodi ya klabu ya Al Ahly Khaled Mortagey ameiambia BBC.

"Mapato yote yalisimama kwa hiyo sasa tutaweza kuishi."

Kulikuwa na wakati watu walikuwa na wasiwasi mkubwa miongoni mwa vilabu kwamba ligi hiyo msimu huu isingechezwa tena.

Kwa mujibu wa Mortagey, wacheza soka wa nchi hiyo pia wamefurahishwa kufahamu ligi yao inarudi tena.

Ligi hiyo ilisimama mwezi wa Januari ikiwa imefikia nusu baada ya wimbi la harakati za kimapinduzi kuikumba Misri.

Vigogo wa Cairo, Zamalek, ambao wanapigania kuutwaa ubingwa wa ligi kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2004, ndio wanaongoza wakiwa na pointi 32, wakiwa mbele kwa pointi tatu dhidi ya Ismaily, baada ya kucheza michezo 15.

Mahasimu wa Zamalek, Ahly, wanaowania nao kushinda ligi kwa mwaka wa saba mfululizo, wanashikilia nafasi ya nne wakiwa na pointi 26.