Mtafaruku Abidjan, Ivory Coast

Mabomu yamelipuliwa katika wilaya moja mjini Abidjan ambayo inampinga Rais Laurent Gbagbo na iliripotiwa kuwa watu wasipungua 10 walifariki dunia.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Mfuasi wa Ouattara akiwa Abobo, Abidjan

Wakaazi katika eneo hilo walisema Bomu moja lililipuliwa katika soko moja maarufu iliyoko Abobo.

Watu wapato 370,000 wamekimbia makwao kuepuka ghasia hizo za hivi karibuni wengi wao wakiwa kutoka Abobo ambayo inamuunga mkono Alassane Ouattara.

Wafuasi wa Bw Gbagbo wamerushiwa shutuma za kuwashambulia wafuasi wa Bw Ouattara, mhasimu wa Bw Gbagbo.

Bado haijulikani ni nani aliyerusha mabomu hayo Abobo.

Mkaazi mmoja aliliambia shirika la utangazaji la AFP "Niliona maiti ya mwanamke mmoja, wanaume 11 na vijana kadhaa kwenye uwanja. Tumetawanyika katika eneo hili. Mimi na watoto wangu ilibidi tuyahame makazi yetu."

Pia iliripotiwa kuwa wanamgambo wanaomuunga mkono Ouattra wamekishambulia kituo cha polisi katika eneo jingine Abidjan.