Man U yachanja mbuga, Arsena yabanwa

Bao la dakika za lala salama la Dimitar Berbatov liliiwezesha Manchester United iliyokuwa na wachezaji 10, kuzoa pointi tatu dhidi ya Bolton na kizidi kujichimbia kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya England, kwa pointi tano dhidi ya Arsenal wanaofuata nafasi ya pili.

Haki miliki ya picha PA

Katika kipindi cha kwanza kilichokuwa na nafasi chache, mkwaju wa Javier Hernandez ulikwenda nje na free-kick iliyopigwa na Martin Petrov ikaokolewa na mlinda mlango Edwin van der Sar.

Jonny Evans alioneshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja katika kipindi cha pili baada ya kumrukia kwa miguu miwili Stuart Holden aliyetolewa nje kwa matibabu zaidi.

Lakini bao la Berbatov limeipatia pointi tatu, Manchester United baada ya mlinda mlango wa Bolton Jussi Jaaskelainen kushindwa kuudaka mkwaju wa Nani na mfungaji akauwahi na kuujaza wavuni.

Kwa matokeo hayo Manchester United imefikisha pointi 63 wakiongoza ligi hiyo.

Arsenal walifaulu kugeuza kibao cha matokeo baada ya kufungwa mabao mawili na West Brom na timu hizo kugawana pointi baada ya kufungana 2-2.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Andrey Arshavin

Wenyeji West Brom walipata bao la mapema baada ya mkwaju wa kona iliyopigwa na Chris Brunt na kumkuta Steven Reid hajakabwa na mchezaji yeyote wa Arsenal na kuujaza mpira wavuni na kumuacha mlinda mlango Manuel Alumnia akigaagaa.

Bao la pili la West Brom liliwekwa wavuni na Peter Odemwingie kwa urahisi katika dakika ya 58 ya kipindi cha pili, baada ya mlinda mlango Almunia na beki wake Sebastian Squillaci kuchanganyana.

Arsenal walijiuliza kipindi cha pili na Arsvani katika dakika ya 70 akaipatia Arsenal bao la kwanza.

Robin van Persie alipachika bao la kusawazisha katika dakika ya 78 na kufanikiwa kugawana pointi moja.

Arsena bao wanaendelea kushikilia nafasi ya pili kwa kufikisha pointi 58 na West Brom nafasi ya 16 wakiwa na pointi 33.

Stoke wameendelea kushikilia rekodi yao ya kutofungwa nyumbani mwaka huu wa 2011, baada ya kupata ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Newcastle katika mchezo uliokuwa wa kuvutia sana.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Wachezaji wa Stoke wakishangilia

Stoke wakicheza nyumbani walipata bao la kwanza baada ya Jon Walters kuunganisha kwa kichwa krosi ya Jermaine Pennant.

Waliongeza bao la pili dakika moja baadae baada ya Pennant kutumia makosa ya mlinda mlango wa Newcastle Steve Harper aliyeshindwa kuokoa mpira.

Danny Higginbotham aliipatia Stoke bao la tatu kwa mkwaju wa yadi 20, kabla ya Ricardo Fuller kuachia mkwaju wa yadi 12 na kuhitimisha idadi ya mabao 4-0.

Matokeo hayo yameifanyanya Stoke kufikisha pointi 37 wakiwa nafasi ya 10.

Wolves walifanikiwa kupata ushindi wao wa kwanza katika uwanja wa Villa Park kwa muda wa miongo mitatu iliyopita na katika jitahada za kujikwamua kutoka mkiani mwa ligi na kuiongezea hofu Aston Villa ya kuteremka daraja.

Image caption Wolves dhidi ya Aston Villa

Wolves walifanikiwa kufunga bao lao hilo moja katika dakika ya 38 na kuipeleka timu hiyo hadi nafasi ya 18 na pointi 33.

Aston Villa wapo nafasi ya 14 lakini pointi zao ni 33, eneo walilopo na pointi zao zinawaletea hofu ya kuwemo katika timu za kushuka daraja.

Maynor Figueroa alifunga bao muhimu katika dakika za nyongeza na kuweza kuipatia ushindi Wigan wa mabao 2-1 dhidi ya Birmingham City ambao nao wamo katika hatari ya kushuka daraja.

Image caption Maynor Figueroa

Wigan wanaoburura mkia walikuwa wa kwanza kufungwa baada ya Liam Ridgewell kuonekana akifunga katika nafasi aliyoonekana ameotea.

Lakini wenyeji waliweza kujiuliza na kujipanga baada ya kuanza kwa kutetemeka na kusawazisha baada ya Tom Cleverley kwa mkwaju wa karibu na lango.

Na ndipo ilipowadia wakati Figueroa alipoipatia bao la ushindi Wigan kwa mkwaju wa yadi 20 ulioiwezesha timu hiyo kufanikiwa kupata pointi 30.

Mpambano mwengine wa kusisimua ulikuwa ni kati ya Blackburn na Blackpool, ambapo timu hizo zilimaliza kwa kufungana 2-2.

Blackburn waliokuwa wenyeji walikuwa nyuma kwa mabao mawili hadi dakika ya 49 ambapo nahodha Samba aliandika bao la kwanza kabla Hoilett kusawazisha mabao ya kipindi cha kwanza yaliyofungwa ba Charlie Adam katika dakika ya 25 na 29.

Haki miliki ya picha b
Image caption Tottenham dhidi ya West Ham

Katika mchezo wa mapema mchana, Tottenham walishindwa kuutumia uwanja wa wao baada ya kulazimishwa sare ya kutofungana na West Ham.

Bado Tottenham wanashikilia nafasi ya tano wakiwa na pointi 49.