Chelsea yaichapa Man City

Chelsea imejikita katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi kuu ya England, baada ya kuichapa Manchester City kwa mabao 2-0.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption David Luiz aliandika bao la kwanza

Wakicheza bila Carlos Tevez, City hawakuonesha cheche zozote, ingawa Yaya Toure aliachia mkwaju mmoja uliookolewa na Peter Cech.

Wakisaidiwa na chenga za Salomon Kalou, Chelsea walifanya mashambulizi baada ya mapumziko, ba beki David Luiz kufunga kwa kichwa, zikiwa zimesalia dakika 12.

Bao la pili lilifungwa na Ramires, alipowapiga chenga mabeki wa City katika dakika za majeruhi na kupachika bao maridadi.

Image caption Luis Suarez

Katika mchezo mwingine, penati yenye utata na uchezaji maridadi wa Luis Suarez umeipa ushindi Liverpool dhidi ya Sunderland.

Sunderland ilifungwa bao la kwanza baada ya mkwaju wa penati uliopigwa na Dirk Kuyt, baada ya John Mensah kumfanyia madhambi Jay Spearing.

Refa Kevin Friend awali alisema upigwe mpira wa adhabu, kabla ya kubadili mawazo na kuufanya mkwaju wa penati, baada ya kumsikiliza mshika kibendera.

Suarez alipachika bao la pili baada ya mapumziko, baada ya kukatiza katika upenyo mdogo.