Wenger afurahishwa kujituma wachezaji

Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger amefurahishwa na namna wachezaji wake walivyopigana kiume na kufanikiwa kutoka sare ya 2-2 na West Brom, wakiwa nyuma ya vinara wa ligi Kuu ya England, Manchester United kwa pointi tano.

Image caption Arsene Wenger

Mabao mawili yaliyofungwa kipindi cha pili, yaliwaokoa Arsenal na kupata pointi moja wakiwa wamesaliwa na michezo tisa. Wenger alisema baada ya mchezo huo: "Kilichopendeza ni namna timu nzima ilivyojituma na kuweza kurejesha mabao.

"Itakuwa ni vuta ni kuvute hadi mwisho kwa sababu tupo tayari kupambana."

Gunners bado wana mechi dhiddi ya Manchester United tarehe 1 mwezi wa Mei katika uwanja wa Emirates.

Wiki chache zilizopita hazikuwa za furaha kwa Wenger na timu yake, baada ya kufungwa katika fainali ya Kombe la Carling, kuondolewa michuano ya Ubingwa wa Ulaya na kupoteza mchezo wa robo fainali ya Kombe la FA dhidi ya Manchester United.

Wakati vijana wa Sir Alex Ferguson walipoteleza hivi karibuni kwa kupoteza mechi mbili mfululizo za ligi, mechi ya Jumamosi ya Arsenal dhidi ya West Brom ilikuwa nafasi nzuri ya kurudisha ari kwao na kuzidi kuweka hai matumaini ya kunyakuwa Ubingwa wa Ligi msimu huu.

Waliianza siku ya Jumamosi wakiwa nyuma kwa pointi tatu na mchezo mmoja mkononi, vijana wa Wenger, walikuwa nyuma kwa mabao 2-0, lakini mabao ya Andrey Arshavin na Robin van Persie kipindi cha pili yaliiwezesha Arsenal kuambulia pointi moja na kuwaruhusu Manchester United kutanua wigo wa pointi na kufikia tano, meneja wa Arsenal ana ari ya kutazama mbele kwa mafanikio zaidi.