I. Coast na Libya mechi zao viwanja huru

Mechi za kufuzu kwa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2012 kwa nchi za Ivory Coast na Libya mwishoni mwa wiki hii, zimepelekwa katika viwanja huru kwa sababu ya machafuko yanayozikumba nchi hizo mbili.

Image caption Kombe la Mataifa ya Afrika

Ivory Coast maarufu kwa jina la Tembo, sasa watakabiliana na Benin nchini Ghana, wakati Libya itapambana na Comoro nchini Mali katika mechi za kundi C.

Ivory Coast awali walipangiwa kucheza katika kundi lao la H siku ya Jumapili mjini Abidjan.

Lakini machafuko yanayotokea nchini Ivory Coast kutokana na uchaguzi mkuu, yamelazimisha mechi hiyo sasa kuchezwa mjini Accra siku ya Jumamosi.

Taarifa ya Rais wa Chama cha Soka cha Ghana, Kwesi Nyantakyi imesema:"Ivory Coast watacheza mechi yao ya Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Benin mjini Accra."

"Tumekubaliana kuwa wenyeji wa mchezo huo mjini Accra, kwa sababu ya hali ya usalama baada ya maafisa wa chama cha soka wa Ivory Coast kutuomba."

"Ni ndugu zetu na tupo tayari kuwasaidia kucheza mechi yao ya kufuzu nchini kwetu wakati wowote watakapohitaji."

Ivory Coast wanatazamiwa kushinda na kuongeza wigo wa pointi katika kundi H watakapokabiliana na Benin.

Tembo hao wanaongoza kundi lao wakiwa na pointi sita baada ya mechi mbili walizocheza.

Benini wanaoshikilia nafasi ya pili wana pointi nne, Burundi wanashikilia nafasi ya tatu wakiwa na pointi moja, huku Rwanda ikiwa haijaambulia pointi hata moja.

Libya watapepetana na Comoro mjini Bamako siku ya Jumapili kwa sababu ya vita vinavyozidi kupamba moto baina ya waasi na wanajeshi watiifu wa Kanali Moammar Gadhafi.