Kenya haitashinda kesi za ICC asema Ocampo

bendera ya kenya

Baada ya baraza la usalama la umoja wa mataifa kukataa hoja ya serikali ya Kenya ya kutaka mahakama ya kimataifa ya ICC ihairishe kesi zinazowakabili watu wanaoshukiwa kuchochea ghasia za baada ya uchaguzi uliopita, sasa Kenya iko mbioni kutafuta njia nyingine.

Na njia pekee iliyopo sasa ni kukata rufaa mbele ya mahakama hiyo. Lakini kiongozi wa mashataka Louis Moreno Ocampo akiwa ziarani London amesema haoni uwezekano wa kenya kufaulu katika hoja hiyo.

Kampeni za majuma kadhaa za serikali ya Kenya za kutaka kuungwa mkono na jamii ya kimataifa ili kesi hizo ziahirishwe zilifikia kikomo siku ya Ijumaa, baada ya kikao cha baraza la usalama la umoja wa mataifa kisichokuwa rasmi, kukataa hoja hiyo ya Kenya.

Sasa hatua pekee iliyosalia kwa Kenya ni kutumia ibara ya 19 ya sheria iliyobuni mahakama ya ICC , inayoruhusu nchi kupinga uamuzi wa mahakama ya ICC.

Hata hivyo Kiongozi wa mashtaka katika ICC Luis Moreno Ocampo anasema ingawa serikali ya Kenya ina haki ya kukata rufaa, haoni uwezekano wa kesi kuahirishwa.

Ocampo aidha aliondolea mbali hofu ya kukamatwa kwa washukiwa hao sita watakapofika mbele ya mahakama ya ICC Mjini The Hague tarehe saba na tarehe nane mwezi ujao. Lakini alikumbusha kwamba yeyote anaweza kukamatwa akiwatishia mashahidi.

Ocampo alikuwa ameiandikia barua serikali ya Kenya akielezea wasi wasi wake kwamba washukiwa wawili - naibu waziri mkuu Uhuru Kenyatta na mkuu wa utumishi wa umma Francis Muthaura wanashikilia nafasi serikalini zinazowapa uwezo kuingilia ushahidi.

Washukiwa wanaotarajiwa kufika mahakamani The Hague tarehe saba mwezi ujao ni aliyekuwa waziri wa elimu ya juu William Ruto, mbunge Henry Kosgey na mtangazaji wa radio Joshua Arap Sang. Bwana Kenyatta, Bwana Mutahura na aliyekuwa mkuu wa Polisi Hussein Ali. Baada ya hatua hiyo , kwa mujibu wa Bwana Ocampo , watasubiri kipindi cha miezi sita kuipa mahakama muda wa kuthibitisha mashtaka.