Misri yaunga mkono mabadiliko ya katiba

Image caption Upigaji wa kura za maoni, Misri

Wamisri wameunga mkono mabadiliko ya katiba yatakayoruhusu nchi hiyo kuharakisha uchaguzi kufanyika.

Matokeo rasmi yameonyesha kuwa asilimia 77 ya wapiga kura katika kura ya maoni iliyofanyika siku ya Jumamosi yameunga mkono mabadiliko hayo.

Chini ya uongozi wa Rais Hosni Mubarak, uchaguzi ulikuwa ukipangwa, matokeo yalikuwa yakijulikana kabla ya hata kupigwa kura kwenyewe na idadi ya watu waliojitokeza walikuwa wachache.

Uchaguzi wa wabunge unaweza kufanyika mapema, huenda ukawa mwezi Septemba.

Mohammed Ahmed Attiyah, mkuu wa kamati ya juu ya kisheria ambaye alisimamia kura hizo, alisema watu milioni 18.5 waliopiga kura waliunga mkono mabadiliko hayo.

Waliojitokeza ni asilimia 41.2 ya wapiga kura milioni 45 waliokuwa na sifa za kupiga kura.

Mabadiliko hayo ni pamoja na:

. Kupunguza mihula ya Urais kutoka miaka sita hadi miaka minne na kumruhusu Rais akae madarakani mihula miwili tu.

.Kumtaka Rais achague naibu katika kipindi cha siku 30 baada ya uchaguzi.

.Kuanzisha sifa mpya za mgombea urais, ikiwemo sheria ya kwamba lazima awe na umri wa zaidi ya miaka 40 na asiwe ameoa mwanamke ambaye si raia wa Misri.

Makundi mawili makuu ya kisiasa, chama cha National Democrat cha Bw Mubarak na Muslim Brotherhood, waliunga mkono mapendekezo hayo.

Msemaji wa kundi la Brotherhood, Essam al-Aryan, aliyaita matokeo hayo "ushindi kwa watu wa Misri", itakayoruhusu nchi "kufungua ukurasa na kuanza upya".