Rais wa Fifa Blatter kustaafu 2015

Sepp Blatter amesema atang'atuka katika nafasi yake ya Urais wa Fifa mwaka 2015, iwapo atachaguliwa tena kwa muhula wa nne mwezi wa Juni.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais wa Fifa Sepp Blatter

Blatter mwenye umri wa miaka 75, ambaye ameongoza Shirikisho hilo la Soka Duniani tangu mwaka 1998, anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Mkuu wa Shirikisho la Soka barani Asia, Mohamed Bin Hammam.

"Unajua ninawania kwa miaka mingine minne," aliuambia mkutano wa Baraza la Uefa siku ya Jumanne. "Lakini hii itakuwa miaka yangu minne ya mwisho kusimama nikiwa nawania kuchaguliwa tena."

Rais mpya atachaguliwa katika mkutano mkuu wa Baraza la Fifa, utakaoanza tarehe 31 mwezi wa Mei.

Huku Bin Hammam akiahidi kuongeza nguvu ya uamuzi kwa Fifa na njia bora zaidi ya wanachama kufaidika na hazina ya Fifa, Blatter anakabiliwa na changamoto yake kubwa ya kwanza tangu Issa Hayatou alipowaniwa na kushindwa mwaka 2002.

Bin Hammam pia anahudhuria mkutano wa Baraza Kuu la soka barani Ulaya- Uefa, akiwa anaitumia nafasi hiyo kuanza kutafuta kura kwa uchaguzi utakaofanyika mjini Zurich tarehe 1 mwezi wa Juni.

Wanachama 53 wa Uefa wa nchi zinazowakilisha zaidi ya robo ya wapiga kura 208 wa Fifa ambao Blatter na Bin Hammam watajaribu kuwashawishi kupata kura zao.