Ferdinand kuendelea kuichezea England

Rio Ferdinand ataichezea England licha ya kupoteza nafasi yake ya unahodha, kwa mujibu wa taarifa za watu walio karibu na mchezaji huyo.

Image caption Rio Ferdinand

Kitengo cha michezo cha BBC, wiki iliyopita kilibainisha uamuzi wa meneja wa England, Fabio Capello kumrejeshea unahodha John Terry, kulimuudhi sana Ferdinand.

Ilielezwa mlinzi huyo, ambaye anauguza maumivu ya mguu kwa muda mrefu, alishtushwa kwa uamuzi huo wa Capello na alikuwa akifikiria mara mbilimbili mustakabali wake katika timu ya taifa.

"Rio kamwe hataipa kisogo England," taarifa hizo zilieleza.

"Anapenda kuichezea nchi yake na Fabio Capello hawezi kubadilisha hilo."

Capello alithibitisha Terry atakuwa nahodha wa England wiki hii wakati watakapocheza na Wales kutafuta nafasi ya kufuzu mashindano ya Euro 2012, pia mechi ya kirafiki dhidi ya Ghana wiki ijayo na mechi nyingine zijazo.

Mlinzi huyo wa Chelsea pamoja na Capello, siku ya Ijumaa wanatazamiwa kuzungumza na waandishi wa habari.

Suala hilo la unahodha lilikuwa likitishia maandalizi ya mchezo wa siku ya Jumamosi dhdi ya Wales mjini Cardiff, ambapo pia kwa mara ya kwanza winga wa Wolves, Matt Jarvis ameitwa katika kikosi cha England.

Ferdinand alionekana kukwepa kukutana na Capello siku ya Jumatano na Jumamosi, wakati meneja huyo alipokwenda uwanja wa Old Trafford kwa ajili ya kuangalia michezo ambayo Manchester United iliyocheza dhidi ya Marseille na Bolton.

Wachezaji wengi wa timu ya taifa ya England inasemekana hawafurahii Terry kurejeshewa unahodha baada ya kuvuliwa kutokana na tuhuma za kuwa na uhusiano wa kimapenzi mwandani wa mchezaji mwenzake wa zamani Wayne Bridge mwaka mmoja uliopita.

Wakati huo Capello aliapa kutomchagua tena Terry kuwa nahodha, lakini matatizo ya kuumia kwa Ferdinand kumesababisha Capello abadili mawazo.