Museveni alaani mashambulizi ya Libya

Rais Museveni
Image caption Museveni anasema nchi za magharibi zinabagua Libya na amependekeza mashambulizi yakome

Harakati za jamii ya kimataifa zinazoendela dhidi ya Libya zimekosolewa Rais Yoweri Museveni wa Uganda.

Katika tahariri yake kuhusu mgogoro wa Libya, iliochapishwa kwenye magazeti nchini humo Rais Museveni amemkosoa na pia kumtetea Kanali Muamar Gaddafi.

Kiongozi huyo amepinga upinzani ambao unaungwa mkono na mataifa ya kigeni na ameyaita mataifa hayo kama yenye undumila kuwili unaothibitishwa na kuweka haraka marufuku ya ndege kupaa kwenye anga ya Libya.

Museveni ambaye ni mmoja walioteuliwa kwenye jopo la kutatua mzozo huo na Umoja wa Afrika amehoji kwa nini nchi hizo zina puuza hali mbaya kama vile ya Bahrain ama maeneo mengine yenye kuegemea upande wa magharibi.

Katika tahariri hiyo, anauliza ikiwa Benghazi pekee ndio kuna raia na Mogadishu hakuna au ni kwa sababu nchini Somalia ambapo wameomba Umoja wa Mataifa kuingilia kati mzozo unaoendelea hakuna mafuta.

Aidha, Rais Museveni amemsifu Kanali Gadafi kama mmoja wa viongozi wa Kiarabu ambae hashabikii uislamu wa itikadi kali.

Kiongozi huyo pia amemsifu Gaddafi kama kiongozi wa Afrika ambaye ana mawazo yake binafsi asie shawishika na sera za kigeni.

Kwenye tahariri hiyo pia, Rais Museveni amekosoa sera za Gaddafi, na kutoa mifano kama alivyounga mkono utawala wa Iddi Amin alieongoza Uganda tangu mwaka wa 1971 hadi 1979.

Museveni ameongeza kuwa Gadaafi alikosa kuingilia mambo ya ndani ya nchi za kiafrika, kwa mfano kwa kuwahusisha viongozi wa kijadi ama kitamaduni, kama vile wafalame na watemi katika masuala ya kisiasa.

Tahriri yake imekamilika kwa kuutaka umoja wa Mataifa kudurusu azimio lake la marufuku ya ndege kupaa kwenye anga ya Libya.