Adebayor kuichezea tena Togo

Soka ya Togo imepokea habari muhimu za kupendeza kwamba kocha Stephen Keshi na mshambuliaji Emmanuel Adebayor wameamua kurejea katika timu ya taifa.

Image caption Emanuel Adebayor

Adebayor anayechezea Real Madrid, aliamua kuacha kuchezea timu ya taifa baada ya shambulio la risasi lililoelekezwa katika basi la wachezaji wa Togo, wakati wa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Angola 2010, ambao watu wawili waliuawa.

Adebayor tayari amelihakikishia Shirikisho la Soka la Togo, atacheza siku ya Jumamosi dhidi ya Malawi katika kundi lao la K.

Kocha Keshi raia wa Nigeria tayari yupo nchini Togo akichukua nafasi ya kocha Mfaransa Thierry Froger.

Keshi alizozana na Shirikisho la Soka la Togo mwaka 2006 baada ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2006.

Lakini Keshi, ambaye bado hajasaini mkataba na Shirikisho la Soka la Togo, anarudi kwa mara ya tatu baada ya Froger kujiuzulu kwa vile amepata kazi ya kuifundisha timu ya Nimes ya Ufaransa mapema mwezi huu.

Adebayor pia alijiondoa kuichezea timu ya taifa ya Togo, miezi mitatu baada ya waasi wa jimbo la Cabinda kushambulia kaskazini mwa Angola na kuleta kizaazaa ambapo timu hiyo ilijitoa katika mashindano ya Mataifa ya Afrika 2010.

"Nimepima tena mawazo yangu kwa muda wa miezi sasa tangu shambulio la Angola," Alisema mwezi wa Aprili mwaka 2010.

"Ni tukio ambalo siwezi kulisahau na nisingependa kukutana nalo tena."

Lakini baada ya kusafiri hadi Madrid kukutana na Adebayor, Rais wa Shirikisho la Soka la Togo, Gabriel Ameyi amesema amepokea habari nzuri kutoka kwa nahodha huyo wa zamani wa Togo na sasa ameamua kumaliza kuisusia timu ya taifa.

Adebayor atasafiri moja kwa moja hadi Malawi akitokea Ulaya kwa ajili ya mechi hiyo.