Majeshi washirika yaungana Libya

Haki miliki ya picha libya rebels car
Image caption Gari la waasi Libya

Watu walioshuhudiwa walisema, majeshi ya kimataifa yameanza mashambulio mapya ya anga karibu na mji uliopo magharibi mwa Libya wa Misrata unaoshikiliwa na waasi.

Awali majeshi yanayomtii Kanali Gaddafi yaliondoka eneo hilo, lakini wakazi wa Misrata walisema wadunguaji wameendelea kuwalenga watu wakiwa juu ya majengo.

Kulingana na taarifa zilizotolewa majeshi ya Kanali Gaddafi pia yalianza kuchakaza mji wa Zintan, karibu na mpaka wa Tunisia.

Mapigano hayo yameanza huku nchi za magharibi zikijadiliana ya nani anaongoza harakati za kuingilia kati mzozo wa Libya, huku Marekani ikipendelea zaidi kukabidhi jukumu hilo kwa majeshi ya umoja wa nchi za kujihami za Ulaya, Nato.

Mkazi mmoja wa Misrata aliiambia Reuters kwa simu: "Asubuhi hii, mashambulio mawili ya ndege yamefanyika kwenye kituo cha kikosi maalum cha Gaddafi.

"Watu wawili waliuawa na wadunguaji saa moja iliyopita katikati ya mji. Miili yao sasa iko hospitali, nimewatembelea muda si mrefu. Ufyatulianaji risasi bado unaendelea."

Daktari mmoja kwenye mji huo aliiambia BBC kuwa wandunguaji walikuwa wakiendelea kuwapiga risasi raia, na kuthibitisha kuwa takriban mtu mmoja alikufa.