Adebayor akanusha kurejea timu ya taifa

Emmanuel Adebayor, amekanusha kwamba atarejea kuichezea timu yake ya taifa ya Togo siku ya Jumamosi dhidi ya Malawi, katika mchezo wa kuwania kufuzu mashindano ya Mataifa ya Afrika.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Emanuel Adebayor

Rais wa Shirikisho la Soka la Togo -TFF- Gabriel Ameyi aliwaambia waandishi wa habari mshambuliaji huyo wa Real Madrid atamaliza mgomo wake wiki hii.

"Sikuahidi chochote kama nitarejea katika kikosi cha Togo katika mchezo na Malawi," Adebayor, ambaye ametajwa katika kikosi cha timu ya taifa, ameiambia BBC.

Hata hivyo kocha wa timu hiy Mnigeria Stephen Keshi, amefika Togo kuchukua nafasi ya Thierry Froger.

Adebayor alijiuzulu kuichezea timu ya taifa ya Togo baada ya basi la timu hiyo kushambuliwa kwa risasi wakati wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Angola 2010, ambapo watu wawili wa timu hiyo waliuawa.

Na baada ya kusafiri hadi Madrid na kukutana na Adebayor, Rais wa TFF Gabriel Ameyi alisema amehakikishiwa na nahodha huyo wa zamani wa Togo, kwamba mwaka mmoja wa kuisusia timu ya taifa umemalizika.

Lakini kauli hiyo imekanushwa na Adebayor, mchezaji wa zamani wa Arsenal na Manchester City.

"Iwapo ningekuwa nakwenda kwa ajili ya mechi Malawi, ningekuwa nimeshafika huko muda mrefu," Adebayor aliiambia BBC.

Alithibitisha:"Ndio Kwanza nimemaliza mazoezi na Real Madrid na hata siendi Malawi kujiunga na kikosi cha Togo."