Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Mwizi kaomba msaada polisi

Polisi nchini Marekani walijibu simu ya mtu aliyekuwa akiomba msaada, na kwenda kukuta mwizi akiwa amekwama juu ya jiko kubwa, kwenye hoteli moja mjini New York.

"Alidhani atakufa" amesema Luteni wa polisi Michael Brown, msemaji wa polisi wa Rotterdam, New York. Mwizi huyo Timothy Cypriani, akiwa amejaa masizi na mafuta, aliomba kuokolewa, baada ya kunasa wakati akijaribu kuingia katika hoteli kupitia bomba la kutolea mvuke la jikoni.

Shirika la habari la Reuters limesema mwizi huyo alipanda mti, na kwenda juu ya paa la hoteli hiyo, baada ya hoteli kufungwa usiku. Bila kujua aliingia kwenye bomba la kutolea mvuke, na kunasa huko, huku mvuke wa moto ukimchoma kutokana na jiko kuwashwa kwa siku nzima. Baada ya kuokolewa, alishitakiwa kwa makosa ya wizi, ukorofi wa kihalifu na makosa ya kukutwa na nyenzo za kufanyia wizi.

Majogoo kudhibitiwa

Baadhi ya majogoo katika jimbo la New Jersey nchini Marekani huenda wakakabiliwa na sheria mpya ya kukutana na kuku.

"Hii ni kuokana na kelele wanazopiga" amesema John Hart, mkulima ambaye amesaidia kuandika sheria mpya za majogoo na kuku, katika mji wa Hopewell. Sheria hiyo itawalazimu majogoo na kuku kukutana kwa siku kumi tu kwa mwaka, na sio zaidi ya usiku tano mfululizo.

Kuwika kwa majogoo ni marufuku katika mji huo mdogo, lakini bwana Hart amesema hatua hiyo itazua tatizo kubwa zaidi. "Kuwika ndio mlio wao wa kimsingi, ni kama ishara ya kuwaamsha kuku na kuwaaambia haya sasa muda umewadia" amesema Bwana Hart. Sheria hiyo imekuwa ikijadiliwa kwa miaka mitatu. Kura ya kupitisha au kuipinga sheria hiyo itapigwa Jumatatu ijayo.

Bwana Hart ameongeza kusema kuwa watu wengi wanadhani jogoo anahitajika ili kuku aweze kutaga mayai, kumbe sivyo, jogoo huhitajika kuyapa mbegu mayai ili vipatikane vifaranga.

Fukuza mwizi bila nguo

Bwana mmoja nchini Australia aliamua kumfukuza mwizi huku akiwa hajavaa nguo zozote.

Bwana huyo Ryan Den, akiwa nyumbani kwake siku ya Jumamosi asubuhi, aliona mwizi akitoka nyumbani mwake akiwa kabeba pochi yake pamoja na compyuta mpakato-- yaani laptop. Bwana Dean ambaye hakuwa amevaa nguo zozote wakati huo, aliamua kuanza kumfukuza mwizi huyo mitaani, na hadi kumkamata.

Baada ya kuchukua vitu vyake, bwana Ryan aliondoka na kurejea nyumbani kwake. "Siamini alitoka bila nguo na kumkimbiza mwizi mtaani" amesema Lauren Busse, mke wa bwana Ryan, ambaye wakati wizi unatokea alikuwa bado amelala. Baada ya purukushani hiyo, mwizi huyo kwa bahati mbaya, au nzuri naye aliangusha pochi yake, jambo ambalo lilirahisisha kazi ya polisi kuweza kumkamata.

Bwana Ryan amesema baada ya kuchukua vitu vyake alimuachia mwizi huyo aende zake, lakini bahati tu haikuwa yake, baada ya kudondosha pochi yake iliyokuwa na kitambulisho na anuani ya mahala anapoishi mwizi huyo.

Jela kukimbia madeni

Bwana mmoja nchini Uchina alifanya ujambazi wa uongo ili afungwe jela, kuepuka madeni yaliyokuwa yakimzonga uraiani. Gazeti la Beijing Morning Post limeripoti juzi Alhamisi kuwa, bwana huyo, aitwaye Zou, akiwa ameshikilia kisu, alitishia kumshambulia bwana mwingine aitwaye Zhang.

Bwana Zhou akiwa na kisu chake saa sita za usiku katika mtaa wa Xiaoguangdong, katika wilaya ya Chaoyang, alimkimbiza bwana Zhou, aliyekimbia moja kwa moja hadi ndani ya kituo cha polisi. Bwana Zou alikamatwa mara moja.

Bwana huyo alipanga kufanya wizi huo ili apelekwe gerezani, na kuwaepuka wanaomdai fedha. Bwana huyo alipata hasara kubwa katika baishara zake, na kwa kuona aibu ya kwenda kuwaomba msaada wazazi wake, aliona bora afanye kosa, ili afungwe.

Mke wa rais kuwa rais bila mume

Mke wa rais wa Guatemala ameamua kutengana na mumewe, kwa sababu mke huyo anataka kugombea urais.

Katiba ya Guatemala inapiga marufuku watu wa karibu wa rais kugombea urais. Msemaji wa mahakama ambapo talaka hiyo itashughulikiwa amesema, Edwin Escobar amesema mchakato wa talaka umeanza, kati ya Sandra Torres de Colom na rais Alvaro Colom, ambaye hawezi tena kuwania urais.

Iwapo mume huyo atakubali kutoa talaka, wawili hao watakuwa wametengana rasmi ndai ya kipindi cha mwaka mmoja. Bi Torres alitangaza mapema mwezi huu kuwa atakuwa mgombea urais kupitia chama kinachotawala, katika uchaguzi utakaofanyika mwezi septemba mwaka huu.

Haijafahamika kama akishakuwa rais atarudiana na mumewe, au katiba pia inakataza hilo.

Na kwa taarifa yako.... Kwa wale wanaojua stempu ni nini -- Uingereza ni nchi pekee duniani ambayo stempu zake hazina jila la nchi

Tukutane wiki ijayo... Panapo majaaliwa.

-----------------------

Habari kutoka mitandao mbalimbali ya habari duniani