Wengi wamwelemea 'mchungaji wa miujiza'

Haki miliki ya picha Michuzi Blog
Image caption Mchungaji Ambilikile "Babu" Mwasapile

Mchungaji mmoja wa Tanzania amewaomba watu waache kwenda kwenye eneo lake la kijijini kupata "tiba ya miujiza" baada ya maelfu ya watu kufurika kwake, na kusababisha vurumai eneo hilo.

Mchungaji Ambilikile "Babu" Mwasapile, mwenye umri wa miaka 76, alisema hataki wateja wengine wapya mpaka siku ya Ijumaa tarehe 1 Aprili, ili mkusanyiko huo wa watu upungue.

Vyombo vya habari nchini humo vimesema takriban watu 52 wamefariki dunia wakisubiri kupata tiba yake.

Mwandishi mmoja wa BBC alisema msururu wa watu umeongezeka hadi kufikia kilomita 26.

Imani za kimiujiza na kupona kwa tiba za asili zimeenea sana nchini Tanzania.

Baadhi ya waganga wa kienyeji walisema viungo vya maalbino ni bora wakati wa kutengeneza hirizi, na kusababisha mauaji ya albino wengi katika miaka ya hivi karibuni.

Dawa ya Bw Mwasapile imetengenezwa na mitishamba na maji, ambapo huiuza kwa shilingi 500 za Kitanzania.

Wataalamu wa kitabibu nchini Tanzania wanafanya uchunguzi iwapo dawa hiyo ni salama na kama ina sifa zozote za kutibu.

Alipomtembelea Bw Mwasapile nyumbani kwake eneo la Loliondo hivi karibuni, mwandishi wa BBC Caroline Karobia aliwakuta watu 6,000 wakimsubiri askofu huyo mstaafu wa kanisa la Kilutherani la Tanzania (ELCT).

Watu husubiri kwa siku kadhaa barabarani na nje ya nyumba yake katika kijiji cha Samunge, bila ya kuwa na mahala pa kulala, maji safi wala vyoo.

Huku taarifa za tiba hiyo zikiwa zimeenea kwa kipindi cha mwezi mmoja uliopita juu ya uwezo wa mchungaji huyo kutibu, imefika hatua ya baadhi ya watu kutolewa hospitali na ndugu zao ambao wanaamini kuwa watatibiwa na Bw Mwasapile.

Baadhi wamekufa kabla hata ya kuonana naye, wakati wengine wameripotiwa kufariki dunia baada ya kunywa dawa yake.

Polisi wa ziada wamesambazwa eneo hilo kudhibiti idadi kubwa ya watu waliojitokeza, baadhi wakiwa wamesafiri kutoka nchi jirani ya Kenya na kwingineko.

Bw Mwasipile aliomba mapumziko hayo kufuatia mkutano na maafisa wa eneo hilo.