Mapigano yazuia watu kanisani I Coast

Vikosi vinavyomtii Rais aliyeshinda katika uchaguzi wa Ivory Coast ambaye pia anaungwa mkono na Umoja wa Mataifa Alassane Ouattara vimeushambulia mji muhimu Daloa wakipiga hatua katika mapigano yenye medani mbili.

Vikosi hivyo vimefanikiwa dhidi ya vikosi vinavyomtii Rais Laurent Gbagbo kwenye medani iliyo mashariki na nyengine iliyo magharibi.

Ikiwa mji wa Daloa utatekwa na wapiganaji wa Ouattara basi hilo litafungua njia ya kufika katika eneo linalozalisha zao la kakao kwa wingi.

Bw Gbagbo bado hakubali kuachia madaraka licha ya Umoja wa Mataifa kusema kuwa alishindwa katika uchaguzi wa mwaka jana.

Haki miliki ya picha none
Image caption Waanaomwuunga mkono Alassane Outtara

Umoja wa Mataifa unakadiria hadi watu 1,000,000 wamekimbia ghasia za Ivory Coast.

Siku ya Jumatatu, wapiganaji wanaomtii Outtara wanaojulikana kama New Forces, walisema kuwa waliuteka mji wa Duekoue, ulio karibu na Daloa, pamoja na Bondoukou ikiwa ni mara ya kwanza kwao kuanzisha shambulio katika maeneo ya mashariki.

Padri mmoja wa huko Duekoue anasema takriban watu 20,000 wameomba hifadhi katika kanisa lake mjini humo, na kuongezea kuomba pande zote zilitazame kanisa hilo kama mahali pa salama kwa wote.

Padri huyo amesema kuwa watu kadhaa wana majeraha ya risasi lakini hawawezi kufika hospitali.

Wengi ni wahamiaji kutoka nchi jirani waliokuwa wakifanya kazi kwenye mashamba ya kakao.

Mamluki wazuiliwa

Mji wa Daloa ndiyo mji mkuu wa mkoa wa Ivory Coast wa magharibi-kati na ndiyo mji mkubwa kuwahi kushambuliwa hadi sasa.

Pindi mji huu utakapotekwa na vikosi vya New Forces basi hatua itakayofuata itakuwa ya mji mkuu wa mkoa, Yamoussoukro, au Pwani ya San Pedro ambao ni muhimu kwa kusafirishia zao la kakao hadi masoko ya nje.

Mwandishi wa BBC John James akiwa katika mji wa Bouake anasema kuwa wapiganaji hao wamefunga mipaka ya nchi yao na Liberia ili vikosi vya Gbagbo visiweze kuajiri askari mamluki kutoka Liberia.

Vikosi hivi, New Forces vimetawala eneo la kaskazini mwa nchi tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 2002.

Wapiganaji wa Gbagbo wameshindwa kila walipojaribu kukabiliana na vikosi hivi tangu uchaguzi wa mwezi Novemba umalizike.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Bw Laurent Gbagbo

Mwandishi wetu anasema kuwa vikosi vya Bw Gbagbo kwa sasa vinakabiliwa na kigezo cha kukabiliana na wapiganaji wa chini kwa chini, maarufu kama Invisible commandos, walioteka sehemu kubwa ya kaskazini mwa mji mkuu Abidjan.

Takriban watu 462 wameuawa tangu mwezi Desemba kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa ambao una askari 9000 wa kuhifadhi amani nchini humo.

Umoja huo umeshutumu wapiganaji wa Gbagbo kwa kurusha makombora katika maeneo wanayoamini yana wafusai wengi wa Bw Ouattara mjini Abidjan, na kusababishia raia wengi kujeruhiwa.

Halikadhalika wapiganaji wanaomtii Ouattara mjini Abidjan nao pia wametuhumiwa kwa kuua wafuasi wa Bw Gbagbo.

Wiki iliyopita Ufaransa ilieneza pendekezo la mswada kwenye Umoja wa Mataifa kutaka Bw Gbagbo na wapambe wake wawekewe vikwazo.

Muungano wa Ulaya tayari umeshachukua hatua kama hiyo, kwa kuchagiza benki maarufu zifunge biashara na hivyo kuathiri biashara ya zao la kakao, ambayo imekuwa tegemeo kuu la mapato ya Bw Gbagbo.