Wamali washangilia wachezaji wa Gaddafi

Haki miliki ya picha harouna traore
Image caption Mashabiki wa mpira Bamako, Mali

Maelfu ya raia wa Mali walijitokeza kuishangilia timu ya Libya katika kufuzu kwa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwenye mji mkuu wa Mali.

Mashindano hayo yalifanyika Bamako kutokana na sababu za kiusalama nchini Libya.

Takriban raia 20,000 wa Mali walijitokeza kushuhudia shindano hilo, wengi wakiwa wamebeba mabango wakipinga uvamizi unaofanywa na nchi za magharibi nchini Libya.

Kapteni Tariq Ibrahim al-Tayib aliiambia BBC baada ya kuichapa Comoro mabao 3-0, "Tumeguswa sana na watazamaji wa Mali"

Mwandishi wa habari aliyopo Bamako Martin Vogl alisema serikali ya Mali ina uhusiano wa karibu na kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi na huungwa mkono sana nchini humo.

Baada ya kila goli katika shindano hilo lililofanyika siku ya Jumatatu jioni, mashabiki hao walikuwa wakiita: "Gaddafi! Gaddafi!," alisema.

Bw Tayib alisema wachezaji wengi hawakuweza kucheza kwasababu walikuwa wanaishi Benghazi, mji ulioshikiliwa na majeshi yanayopambana na Kanali Gaddafi.

Lakini alisema hakuna mgawanyiko wowote wa kisiasa upande wa timu ya soka ya taifa.

Alisema, "Timu nzima inamwuunga mkono Muammar Gaddafi".

Siku ya Ijumaa, maelfu ya Walibya walipita mitaa ya Bamako kuonyesha nia yao ya kumwuunga mkono kiongozi huyo wa Libya- wakiandamana kuelekea kwenye mabalozi ya Ufaransa na Marekani kupinga nchi hizo kujihusisha katika harakati za kijeshi dhidi ya Kanali Gaddafi.