Capello amtaka Carroll ajibidiishe sana

Kocha wa England Fabio Capello, anaamini mshambuliaji Andy Carroll bado hajarejea katika kiwango chake cha kawaida, licha ya kufunga bao lake la kwanza kwa England, walipotoka sare ya 1-1 dhidi ya Ghana.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Andy Carroll

Matamshi hayo ya kocha wa England, ameyatoa siku moja tu baada ya kubainisha alizungumza na Carroll akimtaka apunguze unywaji wa pombe.

"Alifunga bao zuri lakini anatakiwa ajibidiishe sana," Capello aliiambia BBC.

"Sio yule yule Carroll ninayemkumbuka, anahitaji mechi nyingi. Natumai atarejea katika kiwango chake cha kawaida katika mechi dhidi ya Switzerland mwezi wa Juni."

"Ni jambo la kufurahisha kuweza kucheza tena na kufanikiwa kufunga bao. Niko hapa na nipo tayari kufunga mabao nikichezeshwa," alieleza Carroll.

Mechi ya kufuzu kwa Kombe la Euro 2012 dhidi ya Uswiss, inasubiriwa kwa hamu kuona mfumo mpya wa uchezaji alioubuni Capello wa 4-3-3, utakavyofanya kazi tena baada ya kuonesha matunda siku ya Jumamosi walipoilaza Wales dhdi ya Wales 2-0 mjini Cardiff na sare dhidi ya Ghana katika uwanja wa Wembley siku ya Jumanne.

Nahodha wa muda wa England Gareth Barry, alisema mfumo huo mpya unaonekana kukubalika na Capello amefanya jambo jema kubadilisha uchezaji wao.