Mkuu wa majeshi I Coast 'aomba hifadhi'

Wizara ya mambo ya nje ya Afrika Kusini imesema, mkuu wa majeshi wa Rais wa Ivory Coast Laurent Gbagbo ameomba hifadhi katika nyumba ya balozi wa Afrika Kusini mjini Abidjan.

Taarifa zinasema, Phillippe Mangou aliambatana na mkewe pamoja na watoto.

Taarifa hizo zimetolewa huku majeshi yanayomtii Rais anayetambuliwa na Umoja wa Mataifa, Alassane Ouattara, wameripotiwa kuwa nje kidogo ya mji mkuu Abidjan.

Bw Gbagbo ameendelea kung'ang'ania madarakani huko Abidjan, licha ya umoja huo kutangaza kuwa alishindwa kwenye uchaguzi wa mwezi Novemba.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Abidjan

Umoja wa Mataifa umepiga kura ya kumwekea vikwazo Bw Gbagbo na washirika wake.

Mwandishi wa BBC John James kwenye mji mkuu, Yamoussoukro, alisema karibu eneo pekee analodhibiti Rais Gbagbo ni Abidjan.

Siku ya Jumatano, majeshi yanayomtii Bw Ouattara yaliuteka mji wa Yamoussoukro, kilomita 240 kaskazini mwa Abidjan, na eneo alipozaliwa Bw Gbagbo la Gagnoa nalo limetekwa.

Watu 1,000,000 wamekimbia ghasia-wengi kutoka Abidjan- na takriban watu 473 wameuawa tangu mwezi Desemba, kulingana na taarifa za Umoja wa Mataifa.