'Bandari ya kakao yatekwa' Ivory Coast

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Majeshi yanayomwuunga mkono Bw Ouattara

Vikosi vinavyomtii Alassane Ouattara vimeiteka bandari ya pwani ya San Pedro, mji muhimu kwa kutuma nje zao la kakao, hii ni kwa mujibu wa wakazi wa mji huo.

Wapiganaji hao walianza hatua yao ya kupambana na vikosi vya Laurent Gbagbo aliyekataa kukubali matokeo ya uchaguzi wa Rais siku ya Jumatatu na tangu hapo wamefanikiwa kuiteka miji kadhaa.

Mwandishi wa BBC anasema kuwa jeshi la Bw Gbagbo kwa sasa linadhibiti sehemu ndogo tu ya nchi.

Umoja wa Mataifa uliomtambua Bw Ouattara kama mshindi wa uchaguzi huo umepitisha kwa kura adhabu ya vikwazo kwa Gbagbo na wapambe wake.

Vikwazo hivi ni kuongezea hatua za awali za kiuchumi zilizochukuliwa na Muungano wa Ulaya pamoja na makundi ya Afrika kama ECOWAS.

Azimio la Umoja wa Mataifa lililopitishwa, liliandaliwa na Ufaransa pamoja na Nigeria linamzuia Bw Gbagbo na mke wake Simone pamoja na washirika wake watatu walio karibu nao ruhsa ya kusafiri popote duniani.

Vikosi vinavyomtii Bw Alassane Ouattara vimetishia kuelekea mji mkuu wa kibiashara wa Abidjan endapo Laurent Gbagbo hatosalimu amri katika muda wa saa tatu.

Waziri Mkuu wa Bw Ouattara, Guillaume Soro alisema vikosi vijulikanavyo kama Republican Forces of Cote d'Ivoire vina sababu, uwezo na nguvu ya kuhakikisha kuwa Bw Gbagbo anaondoka madarakani.

Ameongezea kusema kuwa hawatolipiza kisasi kwa wafuasi wa Gbagbo na kwamba watafuata sheria kwa kila aliyetenda uhalifu dhidi ya raia wa Ivory Coast.

Takriban watu milioni moja wamekimbia ghasia -wengi kutoka mji mkuu Abidjan na hadi watu 437 wameuawa katika ghasia hizi, kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa.