Majeshi ya washirika 'yaua raia' Libya

Raia saba wamekufa na wengine 25 kujeruhiwa, wakati majeshi ya anga ya washirika dhidi ya msafara wa wanajeshi wanaomuunga mkono Kanali Gaddafi, katika eneo linalodhibitiwa na waasi nchini LIbya, amesema daktari mmoja akizungumza na BBC.

Image caption Silaha za waasi Libya

Daktari Suleiman Refradi amesema shambulio hilo la Jumatano, lilitokea katika kijiji cha Zawia el Argobe, kilomita 15 kutoka Brega.

Shambulio hilo liliteketeza gari lililokuwa limebeba milipuko, na matokeo yake lililipuka na kuteketeza nyumba mbili zilizokuwa karibu.

Wote waliokufa walikuwa na umri wa kati ya miaka 12 na 20, amesema Dokta Refardi. Nato imesema inachunguza tukio hilo.

Taarifa hizi zimekuja wakati kiongozi wa upinzani Mustafa Abdul Jalil akisema waasi watakubali kusimamisha mapigano iwapo wanajeshi wa Kanali Gaddafi wataondoka katika miji mikuu.

Haki miliki ya picha none
Image caption Mustafa Abdul Jalil

"Tunakubaliana na kusimamisha mapigano kwa masharti kuwa ndugu zetu katika miji ya magharibi wawe na uhuru wa kuzungumza, na pia majeshi yaliyozingira miji hiyo yaondoke," Amesema kiongozi huyo katika mkutano na waandishi wa habari, katika mji wa Benghazi.

Daktari Refardi ameiambia BBC kuwa shambulio la Jumatano la majeshi ya washirika lililenga lori na tela lake katika mtaa mmoja mjini zawia el Argobe.

Mlipuko kutoka katika gari hilo ulisababisha vifo hasa kutokana na vipande vya chuma vilivyokuwa vikirushwa.

Wanne kati ya waliokufa ni wanawake, wakiwemo watoto watatu kutoka familia moja, wakiwa na umri wa miaka 12 hadi 16, anaripoti Ben Brown wa BBC akiwa Brega.

Wavulana watatu wenye umri wa miaka 14 na 20 pia waliuawa.

Maafisa wa Nato wameiambia BBC kuwa wanafanya uchunguzi " kutazama mtiririko wa matukio kutafuta iwapo kuna taarifa zinazothibitisha madai haya".

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii