Vidic kurejea, Boateng nje

Beki wa kati wa Manchester United Nemanja Vidic atarejea uwanjani siku ya Jumamosi katika mchezo wa ligi kuu ya England dhidi ya West Ham. Vidic alikuwa na jeraha la misuli kwa muda.

Hata hivyo Rio Ferdinand bado hajapona kuweza kurejea.

Image caption Nemanja Vidic

Mshambuliaji wa West Ham Frederic Piquionne naye anatarajiwa kucheza, baada ya kuumia kidole gumba cha mguu na kusababisha kuukosa mchezo dhidi ya Tottenham.

Wakati huohuo, beki wa Manchester City Jerome Boateng huenda asicheze msimu wote uliosalia kutokana na jeraha la goti.

Meneja wa City Roberto Mancini amesema Boateng atahitaji kufanyiwa upasuaji, na labda akaweza kucheza mechi mbili za mwisho za msimu.

Beki huyo Mjerumani alipata jeraha hilo wakati akichezea timu yake ya taifa siku ya Jumamosi.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Jerome Boateng

Manchini alikuwa na matumaini na jeraha la Micah Richards, kuwa huenda akawa mzima kucheza mechi dhidi ya Manchester United katika nusu fainali ya kombe la FA.

Jeraha la Boateng ni pigo kwa matumaini ya City kumaliza katika nafasi ya nne, nafasi ambayo itasababisha timu hiyo kucheza ligi ya klabu bingwa ulaya msimu ujao.

Man City kwa sasa iko katika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi kuu, pointi nne juu ya Tottenham, lakini wamecheza mchezo mmoja zaidi.