Hatimaye rekodi ya Mourinho yavunjwa

Rekodi ya miaka tisa ya Jose Mourinho kutofungwa nyumbani katika mechi za ligi kwa timu anazoziongoza, ilifikia kikomo baada ya timu yake ya Real Madrid kufungwa bao 1-0 na Sporting Gijon kwenye uwanja wa Bernabeu.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Jose Mourinho

Miguel de Cuevas katika dakika ya 79 alitikisa nyavu za Real Madrid na kuwapa wageni pointi tatu muhimu katika ligi ya Hispania, maarufu La Liga na kumvurugia rekedi yake Mourinho aliyoiweka katika mechi 151.

Kocha huyo raia wa Ureno, msimu huu timu yake imeshinda mara 23 nyumbani, baada ya kuweka rekodi ya kutofungwa nyumbani alipokuwa akifundisha Inter Milan na Chelsea.

Mechi ambayo alifungwa nyumbani akiwa kocha, ilikuwa ni mwaka 2002, wakati Porto ilipolazwa mabao 3-2 na Beira-Mar.

Matokeo dhidi ya Gijon yalikuwa sawa na shubili, kwani ni pigo kubwa kwa matumaini ya ubingwa ya Real Madrid, wakiwa sasa nyuma kwa pointi nane dhidi ya vinara wa ligi hiyo Barcelona.

"Kimahesabu hatujapoteza ligi lakini kwa vile sasa mwanya umefikia pointi nane, inaonekana ni vigumu", alisema Mourinho.

Bahati ni sehemu ya mchezo wa soka na wapinzani wetu Gijon walikuwa nayo na sisi bahati haikuwa upande wetu, alizidi kusisitiza Mourinho.