Ghasia zachelewesha ligi ya Misri kuanza

Ligi ya Misri imeahirishwa kwa muda usiojulikana, siku moja tu baada ya ghasia kuibuka na kuvuruga mechi ya kimataifa mjini Cairo.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Ghasi uwanjani Cairo

Ligi hiyo ilipangwa kuanza upya tarehe 13 mwezi huu wa Aprili, lakini ghasia zilizosababishwa na mashabiki katika mchezo wa siku ya Jumapili kati ya Zamalek na Club Africain, zimelazimisha kuchukuliwa uamuzi huo.

Rais wa Chama cha Soka cha Misri (EFA) Samir Zaher, alitoa tangazo la kuahirishwa ligi hiyo siku ya Jumapili mjini Cairo.

Wajumbe wa EFA watakutana na vilabu siku chache zijazo kutathmini hali ilivyo.

Serikali ya Misri ilifikia uamuzi huo baada ya umati wa mashabiki wa soka kuuvamia uwanja na kulazimisha mechi hiyo ya kuwania Ubingwa wa Vilabu vya Afrika mjini Cairo kusimamishwa.

Wenyeji Zamalek walikuwa wakiongoza kwa mabao 2-1 dhidi ya klabu ya Tunisia ya Club Africain katika hatua ya mkondo wa pili baada ya mchezo wa awali mjini Tunisia, Zamalek kupoteza kwa kufungwa mabao 4-2 wiki mbili zilizopita. Katika mchezo huo wa Cairo, Zamalek walikuwa wanahitaji bao moja tu kuweza kusonga mbele.

Zamalek mabingwa mara tano wa vilabu barani Afrika, walidhani wamepata bao wakati Ahmed Gaafar alipopiga mpira wa kichwa na kujaa wavuni na bao hilo likakataliwa na waamuzi kutoka Algeria kwa vile mfungaji alikuwa amezidi. Katika marudio kupitia picha za televisheni zilionesha kweli mfungaji alikuwa amezidi.

Hatua hiyo ndio iliibua hasira miongoni mwa mashabiki wachache walioamua kuuvamia uwanja na baadae kundi kubwa na mashabiki wakaamua kuwaunga mkono na walinzi waliovalia mavazi ya kimichezo wakafanikiwa kuwalinda waamuzi kabla ya kuwatoa nje ya uwanja.

Waandalizi wa michezo hiyo ya Ubingwa wa Afrika, wanaonekana huenda wakawapatia ushindi Club Africain, wakati Zamalek wanaweza kukabiliwa na adhabu kadha, ikiwemo kutozwa faini na kulazimishwa kucheza mechi zao zijazo za mashindano ya Afrika nje ya Cairo bila watazamaji.

Misri ilikuwa imejipanga kuanza upya ligi yao inayoshirikisha vilabu 16, baada ya kusimama kwa miezi mitatu kutokana na ghasia za kimapinduzi zilizomuondoa madarakani Rais Hosni Mubarak.