Rooney akabiliwa na adhabu kwa kutukana

Wayne Rooney anakabiliwa na adhabu ya kukosa mechi mbili, kutokana na kosa la kutumia lugha chafu wakti Manchester United ilipokutana na West Ham.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Wayne Rooney akitukana mbele ya kamera

Mshambuliaji huyo wa United alitukana mbele ya kamera iliyokuwa ikirusha picha za moja kwa moja, baada ya kupachika bao la tatu kwenye uwanja wa Upton Park.

Mashambuliaji huyo pia wa England ana mpaka Jumanne jioni kukata rufaa dhidi ya shitaka hilo la chama cha soka cha England.

Iwapo atakiri kosa hilo, atapatiwa adhabu hiyo ya kutocheza mechi mbili, lakini iwapo atakana mashitaka hayo, shauri lake litasikilizwa siku ya Jumatano.

Adhabu ya kukosa mechi moja itamkosesha kucheza dhidi ya Fulham siku ya Jumamosi, huku akipatiwa adhabu ya mechi mbili, atakosa mchezo wa nusu fainali ya kombe la FA dhidi ya Manchester City, kwenye uwanja wa Wembley Aprili 16.