Ngome za Gbagbo zapigwa bomu Ivory Coast

vikosi vinavyomuunga mkono Bw Ouattara Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Vikosi vinavyomuunga mkono Ouattarra vimeimarisha mashambulizi dhidi ya Gbagbo

Ndege za kijeshi za Ufaransa na za Umoja wa mataifa zimeshambulia kambi za kijeshi zinazotumiwa na Laurent Gbagbo mjini Abidjan.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Hamadoun Touré amesema ndege hizo zimelenga kuharibu makombora yanayotumiwa na jeshi la Gbagbo dhidi ya raia na vikosi vya umoja wa mataifa.

Mkaazi mmoja mjini Abidjan aliyeshuhudia harakati hizo za wanajeshi wa Ufaransa na Umoja wa Mataifa amesema nyumba yake ilitikiswa na mabomu hayo.

"Nilikuwa nyumbani mwangu, kisha nikasikia helicopter ya kijeshi ikipaa chini sana, ilinibidi nitoke nje kutizama ndipo nikaona ilikuwa ya jeshi la ufaransa. Kisha baada ya muda wa saa moja hivi nikasikia mrindimo wa mabomu na nyumba ikawa inatikisika."

Mkaazi huyo amesema kambi ya kijeshi ya Aqedo ilikuwa inashambuliwa. Na ameelezewa na wenzake kutoka sehemu zingine mjini Abidjan kuwa wao pia wamesikia sauti za milipuko kwenye kambi za kijeshi.

Kwa upande wake waziri wa mashauri ya kigeni katika serikali ya Laurent Gbagbo, Alcide Djedje ameiambia BBC kuwa wanajeshi wa umoja wa mataifa na wale wa ufaransa wanashambulia raia.

Madai hayo yamekanushwa na Umoja wa Mataifa.

Navyo vikosi vinavyomuunga mkono Alassane Ouattarra vimeongeza juhudi zao za kudhibiti mji wa Abidjan.

Waziri mkuu Guillaume Soro amesema sasa wapo kwenye mkondo wa mwisho na katika siku chache tuu watadhibiti utawala wa Ivory coast.

"Tumefurahishwa na harakati za wanajeshi wetu. Mpango ulikuwa kuuzingira mji wa Abidjan na wamefaulu vizuri sana." amesema Waziri Mkuu Soro.

Wakaazi wengi mjini Abidjan wamelazimika kujifungia nyumbani na hawana vyakula, maji na huduma ya umeme.