Vilabu Kenya vyapewa haki ya kupiga kura

Mfumo mpya wa kupiga kura utatumika kumchagua mkuu wa Shirikisho la Soka nchini Kenya, katika jitahada za kuondoa ufisadi.

Kwa mara ya kwanza vilabu vyote vya soka vilivyosajiliwa nchini Kenya, vinavyofikia 3000, vitakuwa na uwezo wa kupiga kura.

Kabla ya hapo ilikuwa ni idadi ndogo tu ya wajumbe waliokuwa wakipata nafasi ya kupiga kura.

"Mfumo huo wa zamani, ulikuwa ukitumiwa kuchagua viongozi wasiofaa, waliokuwa wakihonga majumbe wawachague," Peter Ogonji, Mkuu wa Bodi Huru ya Uchaguzi nchini Kenya(IEB) ameiambia BBC.

Kampuni inayosimamia soka nchini Kenya, Football Kenya Limited (FKL), inayotambuliwa na Fifa kuwa ndiyo rasmi inayosimamia mchezo wa kandanda nchini humo, inatazamiwa kufanya uchaguzi wa mwenyekiti wake mwezi huu.

Maafisa wa Shirikisho la Soka la Kenya, Kenya Football Federation (KFF), wapinzani wa FKL, pia wanaruhusiwa kugombea.

Kuna matumaini makubwa uchaguzi huo utamaliza miaka kadha ya ubishi na migogoro, iliyosababisha kuporomoka maendeleo ya mchezo wa soka nchini humo.

Uchaguzi huo utasimamiwa na Tume ya uchaguzi ya Kenya, inayosimamia pia uchaguzi wa kisiasa nchini humo, ingawa tarehe maalum haijapangwa.

Wagombea katika nafasi ya mwenyekiti kwa FKL, watatakiwa kuonesha " hati maalum juu ya mwenendo mwema " kutoka Idara ya Upelelezi wa makosa ya jinai ya Kenya, alisema, Ogonji.

"Tunataka kumpatia kila mmoja nafasi ya kugombea nafasi illiyopo, lakini wakati huo huo watakaogombea nafasi hizo ni lazima wawe viongozi wanaoaminika."

Ogonji amekiri kwamba maafisa wa IEB bado wanajadiliana na maafisa wa Fifa juu ya idadi ya kura kwa kila klabu.

Fifa inaaminika inapendelea kila klabu kuwa na kura moja tu, wakati IEB wao wanavutiwa na kura tatu kwa kila klabu.