Redknapp asema Spurs hawana wasiwasi

Meneja wa Tottenham Harry Redknapp, amesema timu yake haina wahka wowote wakijiandaa usiku wa leo kuikabili Real Madrid katika mchezo wao wa awali wa robo fainali kuwania Ubingwa wa Vilabu barani Ulaya.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Wachezaji wa Tottenham mazoezini

Spurs wanaocheza mashindano hayo kwa mara ya kwanza, wanakabiliana na mabingwa mara tisa wa vilabu vya Ulaya.

"Sisikii hofu yoyote. Hakuna aliyetutarajia kufikia hatua hii tulipoanza msimu na tunayo nafasi nzuri ya kushinda," alisema Redknapp.

"Hatukuja hapa kusindikiza, tunachotaka ni kupiga hatua ya kusonga mbele."

Hadi sasa Tottenham imefanikiwa vizuri katika ndoto yao katika msimu wao wa mwanzo wa mashindano ya Ulaya, kwa kushikilia uongozi katika kundi lao lililojumisha pia timu za Inter Milan, Werder Bremen na FC Twente, na baadae wakafanikiwa kuwatoa AC Milan bila kufungwa bao hata moja katika mechi zote mbili.

Na kwa kuwa fainali za mwaka huu za Ubingwa wa Ulaya zitafanyika katika uwanja wa Wembley, London, Redknapp amesema hakuna sababu kufikiria harakati zao zinafikia ukingoni.

"Ndoto yetu bado ipo pale pale na hatuna budi kuifanya ndoto yetu hiyo kuwa kweli," aliongeza Redknapp. "Tunakusudia kufika hatua hadi ya mwisho iwapo tutaweza. Tunaelewa ugumu wa mashindano haya, lakini bado tunayo nafasi na hatutaipoteza."