Adebayor aonesha nia ya kubakia Madrid

Emmanuel Adebayor ana matumaini mabao yake mawili katika ushindi wa mabao 4-0 wa Real Madrid dhidi ya Tottenham Hotspur, yatamsaidia kumpatiwa mkataba wa muda mrefu katika klabu hiyo.

Adebayor.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Emanuel Adebayor

Mshambuliaji huyo ambaye ameshafunga mabao matano katika mechi 13 alizokwichazea Real Madrid, yupo kwa mkopo akitokea Manchester City hadi mwisho wa msimu.

"Nimebakiza miezi miwili na klabu ndiyo itakayoamua wanachotaka kufanya - lakini bila shaka ninapendelea kubakia Madrid," alisema Adebayor.

"Ninatakiwa kucheza kwa bidii kila siku na pia kujibidiisha mazoezini.

"Walinileta hapa kusaidia klabu hii wakati msimu ukielekea ukingoni - na leo nimefanya kazi nzuri."

Kocha wa Madrid Jose Mourinho, alimtaka Adebayor wakati Gonzalo Higuain alipoumia na wakati huo huo Karim Benzema akiwa anachechemea.

Higuain alirejea kucheza siku ya Jumanne, wakati Benzema kwa sasa ameumia baada ya kucheza soka safi na kufunga mabao kwenye mechi za karibuni kabla ya kuumia.

Adebayor ameshafunga mabao kumi dhidi ya Spurs - manane akiwa ameyafunga alipokuwa akiichezea Arsenal, mahasimu wakuu wa Tottenham kaskazini mwa London.

"Ninakuwa na furaha sana ninapocheza dhidi ya Spurs, kwa vile mara zote ninakuwa na nafasi ya kuwafunga," Adebayor ambaye alikuwa nahodha wa timu ya taifa ya Togo alibainisha.

"Kwa hiyo hivi sasa tunajiandaa kwa mchezo wa marudiano wiki ijayo na tutafanikiwa kusonga mbele katika hatua ya nusu fainali."

Mchezo wa marudiano utafanyika tarehe 13 mwezi huu wa Aprili, ambapo mshindi atakumbana na ama Barcelona au Shaktar Donetsk katika nusu fainali.