Liverpool kuwakosa Agger na Johnson

Liverpool imepata pigo mara mbili kutokana na kuumia walinzi wake wawili Daniel Agger na Glen Johnson.

Image caption Liverpool

Agger alitoka uwanjani akichechemea siku ya Jumamosi wakati Liverpool ilipolazwa mabao 2-1 na West Brom akisumbuliwa na maumivu ya goti yatakayomlazimu kutocheza soka hadi msimu huu utakapomalizika.

Johnson naye hatacheza soka takriban kwa mwezi mmoja akisumbuliwa na maumivu ya misuli, pia aliumia katika kipindi cha kwanza katika mchezo dhidi ya West Brom.

Mlinzi mwengine wa Liverpool Fabio Aurelio, ameanza mazoezi baada ya kusumbuliwa na maumivu ya misuli.

Aurelio anarejea kwa wakati ambao klabu hiyo itakuwa inahitaji huduma yake, baada ya kutocheza soka kwa muda wa mwezi mmoja.

Meneja wa Liverpool Kenny Dalglish pia ameongezewa nguvu baada ya kurejea kwa kiungo Jonjo Shelvey, ambaye ameanza mazoezi baada ya kupona vizuri upasuaji aliofanyiwa wa goti mwezi wa Februari.

Hata hivyo, kumkosa Agger na Johnson kutaifanya Liverpool kuwa na walinzi wachache wa kutumainiwa hadi kumalizika kwa msimu.

Walinzi hao wawili wa pembeni huenda wasicheze michezo minne ya ligi ambayo Liverpool inajiandaa - mchezo wa nyumbani dhidi ya Manchester City siku ya Jumatatu, safari ya Emirates kuikabili Arsenal siku sita baadae na michezo ya nyumbani dhidi ya Birmingham na Newcastle, tarehe 23 mwezi huu na tarehe 1mwezi wa Mei.