Washukiwa wa Kenya mahakamani The Hague

Washukiwa wakuu wa ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 nchini Kenya wanafika mbele ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC, kwa mara ya kwanza leo.

Image caption Ghasia baada ya uchaguzi wa 2007

Miongoni mwa washukiwa hao sita ni naibu waziri mkuu Uhuru Kenyatta, aliyekuwa waziri wa elimu ya juu William Ruto na mkuu wa utumishi wa umma Francis Muthaura.

Wengine ni mbunge Henry Kosgey, aliyekuwa mkuu wa Polisi Hussein Ali na mtangazaji wa redio Joshua Arap Sang.

Image caption Watu zaidi ya 1000 waliuawa

Watu wasiopungua 1,200 waliuwawa na wengine 500, 000 wakapoteza makazi yao kwenye ghasia hizo.

Mashitaka

Mahakama ya ICC imeeleza kwenye wavuti wake kuwa washukiwa wanatakiwa kufika mbele ya mahakama kwa ajili ya kuthibitisha utambulisho wao, kuhakikisha wamefahamishwa kuhusu uhalifu inaodaiwa waliufanya, na pia kuhusu haki walizo nazo chini ya sheria ya mkataba wa Roma iliyoanzisha mahakama ya ICC.

Ruto, Kosgey na Sang wanatazamiwa kufika mbele ya mahakama leo saa tatu asubuhi kwa saa za Uholanzi, ilhali Bwana Kenyatta, Muthaura na Hussein Ali wanatazamiwa kufika mbele ya mahakama siku ya Ijumaa saa nane alasiri.

Baadhi ya mashtaka yanayowakabili ni mauaji, kuwahamisha watu kwa lazima, ubakaji, udhalilishaji na kuwatesa watu wakati wa ghasia hizo.

Image caption Rais Kibaki na waziri Mkuu Odinga

Ghasia hizo za nchini Kenya zilizuka kufuatia madai kwamba wafuasi wa Rais Mwai Kibaki walikuwa wanajaribu kuiba kura.

Hali ilitulia baada ya makubaliano ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa, ambapo Bw Kibaki alichukua nafasi ya urais huku Bw Odinga akishika wadhifa wa Waziri mkuu.

Kwenye makubaliano hayo yaliyoongozwa na aliyekuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Koffi Annan, washukiwa walitakiwa kushtakiwa katika mahakama za nchini Kenya, na ikishindikana kesi zipelekwe katika mahakama ya ICC.

Mauaji

Mahakama ya ICC inadai kwamba Bw Ruto na Bw Kosgey ambao walikuwa miongoni mwa viongozi wakuu wa chama cha Orange Democratic Party ( ODM) wakati wa ghasia hizo walipanga njama za kihalifu mkoani Rift Valley za kuwashambulia watu waliotambulika kama wafuasi wa chama cha Party of National Unity (PNU).

Mtangazaji Joshua Arap Sang naye anatuhumiwa kushiriki njama hizo kwa kutumia kipindi chake cha redio kuwakusanya wafuasi na kutoa ishara kwa washiriki wengine wa mipango hiyo kuhusu wakati na mahali pa kufanya mashambulizi.

Bw Kenyatta, Bw Muthaura na Bw Hussein Ali wanatuhumiwa na mahakama ya ICC kwa makosa ya mauaji, kuhamisha watu kwa lazima, kuwatesa watu na ubakaji.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Mwendesha mashitaka wa ICC Moreno Ocampo

ICC inadai nguvu za kupindukia zilitumika katika kujaribu kuzima machafuko, na kwamba mpango ulifanyika wa kuagizia kundi lililopigwa marufuku la Mungiki kufanya mashambulizi ya kulipiza kisasi.

Wakati huo huo, mahakama hiyo ya ICC imekataa ombi lililowasilishwa na serikali ya Kenya la kutaka hoja ya kupinga uhalali wa kesi zinazowakabili washukiwa hao sita isikilizwe kwa wakati mmoja na kesi hizo.

Kwa niaba ya serikali ya Kenya, mawakili wawili kutoka Uingereza Sir Geoffrey Nice na Rodney Dixon waliwasilisha mbele ya mahakama hiyo hoja ya kupinga uhalali wa kesi za washukiwa hao sita, kwa madai kwamba idara ya mahakama nchini Kenya haijashindwa kushughulikia kesi hizo.

Serikali ya Kenya

Serikali ilitaka ipewe fursa ya kuzungumza mbele ya mahakama wakati wa kufikishwa kwa washukiwa hao sita.

Lakini majaji watatu wa mahakama hiyo Ekaterina Trendaflova, Hans-Peter Kaul na Cuno Tarfusser walitoa uamuzi kwamba serikali ya Kenya haimo katika kesi hiyo, na kwa hivyo haiwezi kupewa fursa ya kuzungumza wakati wa kesi za washukiwa.

Badala yake waliitaka serikali ya Kenya kuandaa taarifa ya maandishi inayotakiwa kuwasilishwa mbele ya mahakama kabla ya tarehe 28 mwezi Aprili.

Image caption Eneo la Eldoret lililochomwa moto

Kenya inataka kesi hizo ziahirishwe ikidai hatua hiyo itaipa muda wa kuunda idara ya mahakama itakayoweza kufanya uchunguzi na kuwashtaki washukiwa kufikia mwezi Septemba.

Mkuu wa ofisi ya Kenya ya shirika la kimataifa la kutetea haki la International Centre for Transitional Justice Njonjo Mue ameiambia BBC kwamba hakuna uwezekano wa Kenya kufaulu katika hatua hiyo.

"Kulingana na mkataba wa Roma, hoja kama hiyo inaweza kukubalika tu ikiwa serikali imeshafanya uchunguzi na kuwafungulia washukiwa mashtaka yanayowakabili mbele ya ICC. Kwa sasa Kenya haijafanya lolote, imepoteza nafasi nyingi.’’ Alisema Bwana Mue.

Karibu wabunge 40 kutoka Kenya wamesafiri kwenda Uholanzi kuwasindikiza washukiwa hao.

Mahakama ya ICC imetenga viti 70 katika ukumbi wa umma kwa ajili ya idadi kubwa ya Wakenya wanaotazamiwa kufika mahakamani kushuhudia kesi hiyo.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii