Man United kutafuta bao la ugenini

Sir Alex Ferguson ameonesha dalili Manchester United inaweza kusonga mbele katika hatua inayofuata ya nusu fainali kuwania Ubingwa wa vilabu vya Ulaya - iwapo watafanikiwa kufunga bao la ugenini katika mchezo wa kwanza wa robo fainali dhidi ya Chelsea kwenye uwanja wa Stamford Bridge.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Manchester United kupangua rekodi ya Chelsea?

Meneja huyo wa Manchester United, atawataka wachezaji wake kushambulia kwa nguvu ili kupata mabao ya ugenini ya kuwaweka katika nafasi nzuri kwa mchezo wa marudio utakaochezwa uwanja wao mjini Manchester.

"Iwapo tutarejea katika mchezo wa marudio utakaofanyika Old Trafford tukiwa na kitu mkononi, haitakuwa rahisi sisi kupoteza mchezo," alisema Ferguson.

"Jina la mashindano linakumbusha upate bao au mabao zaidi ya moja ya mchezo wa ugenini."

Ferguson ameongeza: "Kwa pambano hili, ninafuraha sana mchezo wa marudio utafanyika Old Trafford. Tutakuwa na wakati mzuri sana katika uwanja wetu."

United inaingia katika mpambano wa Jumatano wakiwa na rekodi ya kutoshinda mchezo wa ugenini dhidi ya Chelsea kwa miaka tisa iliyopita. Tarehe 1 mwezi wa Machi, walifungwa mabao 2-1 katika uwanja wa Stamford Bridge, kwenye pambano la Ligi Kuu ya England na nahodha wao Nemanja Vidic alitolewa nje kwa kadi nyekundu.

Ferguson ametupilia mbali kumbukumbu hizo za historia na kuongeza: "Miaka michache iliyopita hatukufanya vizuri kwa upande wa matokeo, lakini tulikuwa tunacheza vizuri."

Lakini Vidic anaamini rekodi ya Chelsea hivi karibuni dhidi ya timu yake inawapendelea Chelsea.